March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar avutiwa na elimu ya fedha maonyesho ya Madini Geita

Na Joyce Kasiki Timesmajira online,Geita

KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Bi. Zena Ahmed Said, ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mjini Geita, ambapo ameeleza kufurahishwa na namna taasisi hiyo inavyotoa elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, Bi. Zena ameshuhudia wananchi mbalimbali wakielimishwa kuhusu mbinu bora za kuwekeza fedha, hususan kupitia dhamana za serikali ambazo zimeelezwa kuwa na faida kubwa kwa wawekezaji wa ndani.

“Kuna watu wana fedha nyingi lakini hawajui jinsi ya kuziwekeza,hapa kwenye maonyesho haya wanapata fursa ya kufundishwa namna bora ya kuwekeza kwenye dhamana za serikali ambazo huwapatia faida nzuri,” amesema Bi. Zena

Aidha, ameeleza kufurahishwa na juhudi za BoT katika kuelimisha umma kuhusu hatari ya utakatishaji fedha, akisema kuwa ni suala linaloweza kuiingiza nchi katika matatizo makubwa ya kiuchumi na kidiplomasia ikiwa halitadhibitiwa ipasavyo.

“Pia wanafundisha jinsi gani ya kujiepusha na utakatishaji wa fedha, kwa sababu ni suala ambalo linaweza kuiingiza nchi kwenye shida. Kwa hiyo elimu ya masuala haya hapa ni muhimu sana,” ameongeza.

Mbali na masuala hayo, Katibu Mkuu Kiongozi amebainisha kuwa elimu inayotolewa na BoT inagusa maeneo mengi ya kifedha yenye manufaa kwa wananchi wa kada mbalimbali, ikiwemo wajasiriamali, wachimbaji wadogo wa madini, na wafanyabiashara wa kati.

Aidha, Bi. Zena amepongeza waandaaji kwa kuhusisha taasisi na wadau kutoka sekta mbalimbali.

“Nimefurahishwa na maonyesho haya, ambayo mbali na wachimbaji na wadau wa sekta ya madini, pia yameshirikisha wajasiriamali kutoka Tanzania Bara na Visiwani, pamoja na washiriki kutoka nje ya mipaka ya Tanzania,” amesema.