April 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katavi yazindua kampeni kukabiliana na udumavu

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi

MKOA wa Katavi umezindua kampeni ya kuhimiza lishe bora kwa wananchi, katika jitihada za kupunguza udumavu wa kiasi kikubwa unaoshuhudiwa mkoani humo.

Uzinduzi huo ni njia moja wapo ya mpango endelevu wa kulikabili tatizo hilo kutokana na kwamba hali ya wananchi wengi kutokuwa na elimu ya kutosha na sahihi juu ya lishe bora katika familia zao.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko akizungumza Aprili 05, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ambapo amesema takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha kuwa kiwango cha udumavu ni asilimia 32.2 mkoani humo jambo ambalo halikubaliki na lazima juhudi za kupunguza tatizo zifanyike.

Akiwa katika ukumbi wa Mpanda Social Hall, Mrindoko amesema hali hiyo siyo ya kuridhisha hivyo wataalamu wa masuala ya lishe, wakuu wa wilaya na wakurungezi wanapaswa kusimamia kwa vitendo kampeni hiyo.

Kiongozi huyo wa mkoa amesema katika kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kula mlo kamili na siyo kula chakula kwa ajili ya kushiba huku mwili ukiwa haujavuna vya kutosha madini, protini na hata vitamin, hali inayopelekea udumavu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Albert Msovela, amesema  takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha udumavu katika mkoa huo ni asilimia 32.2 sawa na watoto 60,730 ambapo ni kiwango cha juu cha wastani wa taifa wa asilimia 30.

Msovela ameeleza kuwa kwa kutambua hali ya udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano katika mkoa huo bado kuna changamoto kubwa, serikali ya mkoa huo ilizindua mpango wa haraka wa kuongeza kasi ya kupunguza udumavu.

Pamoja na mpango huo na kuunda kamati kuu na sekretarieti hadi hivi sasa baadhi ya shughuli zilizopangwa kutekelezwa zimekamilika kama vile maandalizi ya utafiti wa lishe ya mkoa yamefikia asilimia 25 ya utekelezaji na mkakati wa muda mrefu wa miaka 10 utekelezaji wake umefikia asilimia 15.

Katibu Tawala huyo wa mkoa amesema baada ya uzinduzi rasmi wa kampeni endelevu ya hamasa ya kutokomeza udumavu na changamoto zingine za lishe utekelezaji wake utaanza haraka ambao ni pamoja na kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mpango wa chakula na lishe mashuleni.

Utekelezaji mwingine ni kuratibu utekelezaji wa uzalishaji wa vyakula vyenye virutubisho kwa asilimia 100 na kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa jamii kupitia vyombo vya habari na vipeperushi.

Mtaalamu wa masuala ya lishe ambaye hakutaka jina lake kuandikwa amesema kuwa udumavu ni matokeo ya utapiamlo mkali unaotokana na mtoto kukosa lishe bora katika kipindi cha siku elfu moja tangu kutungwa kwa mimba.

Ambapo amesisitiza mapambano dhidi ya udumavu lazima yaanze katika siku elfu za kwanza za binadamu “ tangu kutungwa kwa mimba  lazima chakula kiwe na uwiano sawa katika kundi la kila chakula na akila kwa usahihi itasaidia kupata mtoto ambaye hajadumaa na itasaidia kuwa na viongozi ambao hawajadumaa katika kufikiri na kufanya maamuzi jambo ambalo tatizo hili tunalo” amesema akicheka.

Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “Lishe Bora, Afya Yako, Zingatia Unacho Kula. Imeelezwa kuwa itachochea hamasa kwa wananchi kuzingatia mlo kamili ambao utapunguza tatizo la udumavu.

Aidha uzinduzi wa kampeni hiyo  unatajwa kuwa ni sehemu ya juhudi za serikali ya mkoa huo kutekeleza agizo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alilotoa mwaka 2024 akiwa Manispaa ya Mpanda wakati ziara yake.