Na George Mwigulu, TimesMajira Online
WARAKA wa Elimu namba mbili wa mwaka 2021 kuhusu urejeshwaji shuleni wa wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali, hasa ujauzito umezidi kufufua matumaini ya wanafunzi waliokuwa wamekata tamaa.
Waraka huo ambao ni matokeo ya uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan umefufua ndoto za wanafunzi wengi ndani ya muda mfupi tangu Waraka huo ulipoanza kutumika mwaka jana.
Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kwa kutambua masuala ya usawa wa kijinsia kwenye upatikanaji wa fursa ya elimu, amefanikisha kurejesha matumaini ya maelfu ya wanafunzi wa kike, ambao ndoto zao za kupata elimu zilikatishwa kwa sababu ya ujauzito huo.
Baadhi yao wanaopata ujauzito sio kwa ridhaa yao, bali kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili hasa kubakwa tena na ndugu wa wakaribu, wakiwemo wazazi.
Mashirika ya kimataifa kwa kutambua vitendo vya ukatili ambavyo wamekuwa wakifanyiwa watoto wa kike hadi kupata ujauzito, ndiyo maana yamekuwa ikimpongeza Rais Samia kwa uamuzi huo.
Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa inayoendelea kufanikisha adhima hiyo ya Rais Samia, licha ya baadhi ya wazazi na walezi kuwa bado hawajawa na mwitikio mzuri kwa ajili ya kuwarejesha masomoni wanafunzi wa kike.
Serikali ya Mkoa huo chini ya utaratibu wa Kuboresha Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP) inatekeleza mpango huo ambapo imeanzisha vituo vitatu vya shule kwa ajili ya kudahili wanafunzi hao.
Tayari vituo hivyo vimedahili wanafunzi 71. Afisa Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Katavi, Beatrice Gati, akizungumza hivi karibuni anasema dira ya elimu nchini ni kuwa na watu walioelimika, wenye maarifa, stadi, uwezo na mtizamo chanya utakaochangia kuleta maendeleo kwa kila mtoto bila kujali jinsi.
Gati ameweka wazi kuwa kutokana na serikali kuongeza fursa na kuboresha elimu kwa ngazi zote kwa kutunga sheria, kanuni, miongozo, lakini jamii inapaswa kuwa sehemu ya kukataa mambo yanayomrudisha nyuma mwanafunzi hususani wa kike.
Akielezea mpango wa SEQUIP, anasema wanafunzi wanaokatiza masomo wazazi na walezi ni chanzo kikubwa cha kushindwa watoto hao kunufaika na elimu, kwani wanakosa ndugu wa kuwaachia watoto ili waendelee na masomo.
“Unakuta mzazi anasema aah! mtoto atamwachia nani. Mimi nina shughuli zangu za kwenda shambani nafanyabiashara… kwa hiyo wanakosa walezi ambao watakuwa waangalizi wa watoto pindi wawapo shuleni,” Anasema Gati.
Anasema wasichana kukata tamaa baada ya kupata ujauzito na ugumu wa maisha unatajwa pia kuwa ni sababu zinazokwamisha kurejea masomoni wanafunzi hao kwa maana baadhi yao baada ya kupata ujauzito wanalazimishwa kuolewa na kuendelea na maisha mengine.
“Wasichana wengi wa kike wanaopata ujauzito wanakata tamaa kwa kuhisi wamefanya makosa makubwa, kubaguliwa na kutengwa na wanafunzi wenzao, ambapo changamoto zote hizo zinawafanya kuathirika kisaikolojia,”anasema.
Ili kuhakikisha mpango wa kuwarejesha masomoni wanafunzi waliopata mimba Katavi unafanikiwa, Mkoa huo umepitisha maazimio Agosti, mwaka huu kwa kutaka kila halmashauri kuanzisha kituo cha wanafunzi wa kike cha SEQUIP na kudahili wanafunzi kuanzia 50.
Tangu uamuzi huo ufikiwe halmashauri tano zitakuwa na wanafunzi hao zaidi ya 250 kuanzia Januari, mwaka ujao.
Mwalimua Idrisa Meru na Mtaalamu wa masuala ya saikolojia ya wanafunzi kutoka Kituo cha Elimu ya Mfumo usio rasmi Kashato, Manispaa ya Mpanda mkoani hapa, anadhibitisha ugumu wa kufanya vizuri kitaaluma w wanafunzi hao kwa sababu ya ushirikiano mbovu kati ya wazazi, walezi na walimu uliopo.
“Mwanafunzi mmoja wa kike alinifuata na kunieleza namna anavyobaguliwa na familia yake kutokana na kupata ujauzito kwa bahati mbaya baada ya mtoto kuzaliwa wazazi wake walimwita ni haramu, lugha ambayo ilimvunja moyo msichana huyo na kuathiri mahudhurio yake darasani”. Anasema.
Licha ya changamoto hizo, anasema hali ya kitaaluma ya wanafunzi hao ni nzuri kutokana na Moduli za masomo wanazotumia zimerahisisha namna ya kujifunza na kwa ushirikiano uliopo kati ya wanafunzi na walimu kwa mtihani ujao wa QT utakao kwa hatua ya kwanza watafaulu kwa asilimia 95.
Akijibu hoja ya mfumo wa elimu usio rasmi kuwa unawatenga wanafunzi na kuonekana kama kundi maalumu, anasema; “Kuna faida kubwa kwenye mfumo huu, kuliko wakosoaji wanavyofikiria, mbali na kusoma masomo ya sekondari waliyokatisha, wanafundishwa masuala mengine yatakayowapa ujuzi na kuendesha maisha yao na kulea watoto wao huku ikiwa ni sehemu nzuri ya kuepuka kubaguliwa na wanafunzi wengine wasio na watoto na kuwaathiri kisaikolojia.”
Kwa upande wa mwanafunzi wa kike wa kituo cha Elimu ya Mfumo usio Rasmi Kashato,Patricia Mpagama anasema zipo sababu zinawafanya wasichana kutorudi shule ambazo ni wazazi kukosa mwamko wa kuwapigania watoto wa kike na badala yake kulenga kuwaozesha, kuwapa jukumu la kuwa walezi wa watoto wa ndugu zao na mazingira mabovu ya kutokuishi na wazazi kwa sababu ya vifo.
Anasema mazingira hayo yamekuwa kikwazo kwa wasichana waliopata ujauzito kutokurudi shule.
“Unakuta binti wa miaka 18 anaishi na bibi yake kwa kuwa wazazi wake walishafariki anaogopa kumwacha bibi yake nyumbani maana yeye ni nguzo ya kuhudumia familia bila kujali umri wake kuwa bado ni mdogo,” anasema Patricia.
Patricia anashukuru Rais Samia kwa mpango huo, kwani ana imani atatimiza ndoto zake za kuwa daktari bingwa, kwani dada yake alishindwa baada ya kupata changamoto inayofanana na yake.
“Lakini mimi nahitaji kuzitimiza ndoto hizo kwa sababu ndoto ya kuwa daktari nilikuwa nayo tangu nikiwa mtoto mdogo,” Anasisitiza Patricia.
Charles Mabula, Mkazi wa Mtaa wa Rungwa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi,kama mzazi anaeleza kuwa suala la wanafunzi kukatizwa masomo hasa kwa kupata ujauzito, wazazi wengi wameshindwa kulipokea na kukubali makosa yanayofanywa na watoto wao, hivyo kukata tamaa ya kuwarudisha shule kuendelea na masomo pindi wanapojifungua licha ya serikali kuweka mfumo mpya wa kuwarejesha shule.
Mabula anasema kuwa mfumo mpya wa elimu bado haujapewa msukumo mkubwa kama ilivyo kwa elimu inayotolewa kupitia mfumo rasmi, ambapo utaona viongozi mbalimbali wa serikali wakitoa matamko makali ya kuhakikisha wazazi na walezi wanaandikisha watoto shule kuanza darasa la kwanza au kidato cha kwanza.
Anasema ili Mkoa Katavi uweze kufikia mpango huo mpya wanapaswa kutoa hamasa kwa nguvu kwenye jamii yote ya Mkoa wa Katavi licha ya kuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza kukwamisha juhudi hizo.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika