Na Respice Swetu, TimesMajira Online, Kasulu
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, inatarajia kufanya bonanza la michezo kwa lengo la kuuaga mwaka wa fedha wa 2021 na kuukaribisha mwaka mpya wa fedha wa 2022.
Bonanza hilo linatarajiwa kufanyika Julai 10 katika chuo cha Ualimu Kasulu likibeba kauli mbiu ya ‘Kazi Iendelee’ ikilenga kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti tangu ameingia madarakani.
Mratibu wa bonanza hilo, Audax Kamugisha amesema kuwa, pamoja na kuuaga mwaka wa fedha unaoisha Juni 30 na kuukaribisha mwaka mpya wa fedha utakaoanza tarehe 1 Julai, bonanza hilo pia litatumika kama jukwaa la watumishi wa halmashauri hiyo katika kufahamiana, kujenga afya na kuoneshana vipaji.
Kamugisha ambaye pia ni mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, amesema michezo itakayohusika katika bonanza hilo kuwa ni mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba na riadha huku mchezo wa riadha ukihusisha kukimbia kwa magunia na kufukuza kuku.
“Tumeziweka timu zitakazoshiriki katika bonanza hilo kwenye makundi manne ambayo ni ya watumishi wa makao makuu ya halmashauri, walimu wa shule za msingi na sekondari, watumishi wa idara ya afya huku kundi la nne likiwa ni la maofisa elimu wa kata, watendaji wa kata na wa vijiji”, amesema Kamugisha.
Sanjari na michezo hiyo, taarifa ya Kamugisha imeweka wazi kuwa, bonanza hilo pia litahusisha fani za ndani za kuimba, vikekesho na uigizaji.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship