December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kasi ya ujenzi Bandari ya Uvuvi Kilwa kielelezo cha Samia kutambua raslimali ya maji ya Bahari

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Kilwa

UAMUZI wa Rais Samia Suluhu Hassan, wa kuamua kujenga mradi wa kielelezo wa Bandari ya Uvuvi Wilayani Kilwa, mkoani Lindi, umeanza kuonesha dalili za kuleta matokeo chanya, baada ya ujenzi wake kufikia asilimia 63.

Bandari hiyo ya uvuvi inayojengwa kwa fedha za ndani ni mradi wa kielelezo unaotekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia. “Mradi huu unatazamwa kama mboni ya jicho letu ili uwe endelevu kwa maana ukikamilika utainua uchumi wa Kilwa, ukanda wa Kusini na Taifa kwa ujumla.

Kutokana na umuhimu wa mradi huo, macho ya viongozi yamekuwa yakifuatilia mradi huo na kulindwa kama mboni ya jicho. Hiyo inadhihirishwa na ziara iliyofanywa juzi na Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, kujionea ujenzi wa mradi huo wilayani kilwa.

Akizungumza jana akiwa eneo la mradi, alisema; “Nimefurahi hatua ni nzuri, tumepiga hatua zaidi ya nusu, muhimu kuhakikisha kazi inakwisha kwa wakati ili Watanzania waweze kuona thamani ya pesa zao, shukrani nyingi kwa Rais Samia kwa kuamua kuujenga mradi huu ambao ni wa kielelezo kwa taifa letu.”

Ulega anasema Bandari ya Uvuvi inayojengwa wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi ni mradi wa kimkakati utakaoleta ajira kwa vijana sambamba na kuongeza pato kwa Taifa.

Ulega anasema tayari ujenzi wake mpaka sasa umefikia asilimia 63 na mpaka kukamilika kwake, ujenzi huo utagharimu sh. bilioni 289 zikiwa ni fedha za ndani za Serikali.

“Nimeridhishwa na ujenzi unavyoendelea, hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 63, na mkandarasi amelipwa asilimia 40. Niwaombe vijana msifanye kazi kwa mazoea, huu mradi tunataka hadi ifikapo Februari 2025 uwe umekamilika na watu wapate ajira,” anasema Ulega.

Anasema mradi huo unapaswa kutazamwa kama mboni kwa kila mpenda maendeleo na ukikamilika utunzwe kusudi uwe endelevu.

Anasema kukamilika kwake utasaidia kuinua uchumi wa Mkoa wa Lindi sambamba na Taifa kwa jumla.

Awali, akizungumzia mradi huo, msimamizi wake kutoka Wizara ya Uvuvi, George Kwandu anasema maelekezo waliyopewa na Waziri Ulega wameyapokea na watayafanyia kazi kwa lengo la kufikia malengo ya Serikali.

“Ametuelekeza mambo mbalimbali ya kufanya ikiwamo ubora wa kazi, kumaliza mradi kwa wakati, watumishi wanaofanya kazi kwenye mradi huu wasiwe na malalamiko,” anasema Kwandu.

Mradi huo ni matokeo ya Rais Samia kutambua umuhimu wa raslimali ya maji katika Bahari, Septemba 19, mwaka jana, aliandika historia mpya katika sekta ya uvuvi baada ya kuweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambayo haijawahi kuwepo tangu nchi ya Tanzania ipate uhuru.

Kukamilika kwa bandari hiyo kutawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Pia, uwepo wa bandari ya uvuvi utachochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi.

Hivyo, uwekezaji huu, unaenda kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kutoka tani 40,721.53 zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 249.54 hadi tani 52,937.99 na kuchangia takriban asilimia 10 katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2036.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, akisisitiza jambo kwa mafunzi wanaojenga bandari ya Uvuvi Kilwa, mkoani Lindi alipokagua ujenzi huo.

Aidha, Bandari hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira kwa Watanzania takriban 30,000, huku katika hatua za awali za ujenzi, jumla ya ajira za muda mfupi 278 zikiwa zimetolewa.

Kati ya hizo, ajira 106 sawa na asilimia 38 zimetolewa kwa wakazi wa wilaya za Mkoa wa Lindi.

Pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Uvuvi, Rais Samia pia aligawa boti 34 kati ya boti 160 ambazo zinatolewa nchi nzima. Boti hizi kwa ukanda wa bahari ya Hindi zipo 92 zikihusisha wavuvi na wakulima wa mwani.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Rais Samia alisema; “Serikali imejipanga kuhakikisha mazingira ya wavuvi na wakuzaji viumbe maji yanaimarika ndio maana anagawa boti za kisasa zikiwa na kifaa cha kuonesha upatikanaji wa samaki na uhifadhi wa samaki,” anasema Dkt. Samia

Moza Salumu, mkazi wa Kilwa Masoko ameishukuru Serikali kwa jitihada za ujenzi wa mradi huo kwa kuwa unakwenda kuwapatia ajira za muda na za kudumu.

“Huu mradi utatusaidia sana hasa sisi vijana na mama zetu, tutapata fursa ya kufanya biashara za aina mbalimbali kwa sababu watu watakuja wengi kutoka sehemu mbalimbali,” amesema Salumu.

Mpaka sasa, vijana 570 wamepata ajira kwenye ujenzi wa mradi huo wa bandari ya uvuvi na imeelezwa utakapokamilikia, vijana 30,000 watapata ajira kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini Tanzania. Sekta ya uvuvi nchini inachangia asilimia 1.8 kwenye pato la Taifa na malengo ya Serikali yanataka ifikapo mwaka 2036/2037 ichangie kwa asilimia 10.

Mradi huo pia unaungwa mkono na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Uwekezaji kwa kuielekeza Wizara kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi wa bandari ya Uvuvi inayojengwa Wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, akionesha alama ya dole gumba kuashiria kuridhishwa na kazi iliyofanyika ya Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Menyekiti wa Kamati hiyo, David Kihenzile , Mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini alisema uamuzi huo wa Serikali ni kwa ajili ya kuongeza Kasi ya uvunaji wa mazao ya bahari na kusaidia ukuaji wa uchumi.

Naye mvuvi Abdallah Ally, anasema utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi nchini, kwa kuwa utaongeza mazao ya samaki yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja na ujenzi wa viwanda.

Aidha, anasema mradi huo utakuwa kichocheo cha uchumi, utaongeza ajira na upatikanaji wa samaki wa kutosha.

“Wote tumemsikia Rais Samia, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara hali ambayo imewavutia wafanyabiashara na wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.