December 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kasi utekelezaji miradi ya maji dhamira ya Samia aliyoanza nayo tangu awamu ya tano

Na Shaban Abdallah, TimesmajiraonlineKigoma

WATU wanaofuatilia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii, wamekuwa wakiona kwa macho yao na kusikiliza shuhuda mbalimbali zinazoelezwa na wananchi jinsi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyoshusha fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mfano, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew anasema Rais Samia
amevunja rekodi kwa kupeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maji kwa akilenga kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi.

Ametoa kauli hiyo wiki hii alipofika Kijiji cha Sisi kwa Sisi kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi mradi wa Maji Sisi kwa Sisi, Kata ya Hale, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

“Katika kipindi ambacho Tanzania imevunja rekodi kwa kushusha fedha nyingi sana mpaka vijijini, ni kipindi cha Dkt. Samia. Katika kipindi ambacho Serikali na Watanzania wako salama, ni kipindi hiki ambacho mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ametutendea haki wanasiasa, ametutendea haki Watanzania, hivyo tunaendelea kujivunia.

Haya yote yanayowezekana sasa yanatupa nguvu ya kufika kwenye miradi. Kama tusingekuwa na fedha tusingeweza kuja na kufuatilia na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali, ni kwa sababu hiyo, Rais amejipambanua, amehakikisha kwamba anatafuta fedha za kutosha ili tuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ili Watanzania waone matokeo kwa vitendo” anasema Mhandisi Mathew.

Mhandisi Mathew anasema yeye na wasaidizi wake kwenye sekta ya maji watahakikisha wanatekeleza miradi yote kwa weledi ili yale malengo ya kufikisha maji kwa wananchi yanatimia.

Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa, anasema Mradi wa Maji Sisi kwa Sisi ulianza kutekelezwa Mei 19, 2022 kwa kutumia Mkandarasi M/s DASKA INVESTIMENT LIMITED wa Mugumu, Musoma.

Lengo la mradi huo ni kutekeleza adhma ya Serikali ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi wapatao 1,035 wa Kijiji cha Sisi kwa Sisi katika Kata ya Hale. Hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 98 na unakusudiwa kukamilika Juni 30, 2024 ingawa wananchi wameanza kupata huduma ya maji kwa majaribio.

Taarifa hiyo inaonesha gharama ya mradi huo hadi kukamilika kwake ni sh. 327,166,478 kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF), ambapo Mkandarasi ameshalipwa sh. 205,040,340 sawa na asilimia 62.7.

“Kazi zilizopangwa na kutekelezwa katika mradi huu ni pamoja na kufunga mitambo ya kusukuma maji. (Water pump & motor) kwa asilimia 99, ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 75,000 kwa asilimia 97, uchimbaji wa mtaro na kufunga mabomba umbali wa mita 5,850 wenye vipenyo vya 3’’, 2.5”, 2’’ ,1.5’’ na 1’’ kwa asilimia 99, ujenzi wa vilula (DPs) sita vya kuchotea maji kwa asilimia 99, ujenzi na usimikaji wa alama za njia ya bomba 90 kwa asilimia 99, na ujenzi wa valvu chemba 12 kwa asilimia 98,” inasema.

Lakini pia katika Mkoa wa Tanga Serikali imetoa sh. Bilioni 25 kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama katika Jiji la Tanga na maeneo ya pembezoni.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, anasema wazi kuwa Rais Samia amepiku kindi cha uongozi wake kwa kupeleka fedha nyingi kwenye halmashauri kwa ajili ya maendeleo.

Kauli hiyo ni uthibitisho wa kipekee unaodhihirisha jinsi Rais Samia amedharia kupeleka maendeleo kwa wananchi. Aidha, viongozi mbalimbali wa Serikali nao wanakiri wao kwamba Rais Samia amepeleka fedha nyingi za miradi katika maeneo wanayoyasimamia.

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu kwenye ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango wakati akizindua hati fungani ya kijani ya miundombinu ya maji Mkoani Tanga, alisema;.

“Namshukuru Rais Sami kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutatua kero za wananchi wa Mkoa wa Tanga katika Sekta ya Elimu, afya, barabara na maboresho ya Bandari ya Tanga.”

Kwa upande wa wakazi wa Kijiji cha Kilelema na Migongo katika Kata ya Kilelema Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wanaridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia kwa kuwa amepeleka neema kubwa ya maji katika kata yao.

Wakizungumza na timu ya waandishi wa habari waliotembelea Kata hiyo juzi kujionea mafanikio waliyopata katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, wameeleza kufurahishwa na dhamira yake ya dhati ya kuwaletea maendeleo.

Kevina Hamis (62) mkulima, mkazi wa Kilelema anasema tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961 wakazi wa Kijiji hicho walikuwa hawajawahi kunywa ya maji ya bomba, lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani neema imewashukia.

“Tangu nchi ipate uhuru tulikuwa tunakunywa na kuoga maji ya mto ambayo siyo salama hali iliyopelekea watoto wetu na watu wazima magonjwa ya ngozi, kuhara mara kwa mara, lakini sasa hatuugui tena,” anasema.

Schola Chishako (45) mjasiriamali, mkazi wa Migongo anaeleza kuwa uongozi wa Mama Samia ni tofauti na marais wengine waliomtangulia, anajali sana maisha ya wakazi wa vijijini, hataki akina mama wateseke ndiyo maana amewapelekea maji.

“Miaka ya nyuma maji ya bomba yalikuwa yanapatikana Mijini tu, lakini tangu aingie madarakani Rais Samia ameleta neema kubwa, maisha ya wakazi wa vijijini hayana utofauti na wakazi wa Mijini, ameleta mageuzi makubwa,” anasema.

Akielezea hali ya huduma ya maji katika Wilaya hiyo, Mtaalamu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani humo, Mhandisi Francis John Molel amemshukuru sana Rais Samia kwa kuwapelekea fedha nyingi sana.

Anasema katika kipindi cha miaka 3 ya Rais Samia huduma ya maji safi ya bomba imefikishwa katika jumla ya vijiji 41 kati ya vijiji vyote 44 vilivyoko katika wilaya hiyo na hata vijiji 3 vilivyobakia mchakato wa kuleta maji umeshaanza.

“Rais Rais ameleta sh. mil 800 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji hapa Kilelema, mradi huu umefika asilimia 45, lakini pia ameshaleta zaidi sh. bilioni 1 kwa ajili ya kutekelezwa mradi mkubwa wa maji katika Kijiji cha Migongo’, alisema.

Anabainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitati ya Rais Samia hali ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama ya bomba katika Wilaya hiyo imeongezeka hadi kufikia asilimia 71 na kabla ya 2025 inatarajiwa kufikia asimia 85,”alisema.

Kwa upande wa Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma Rais Samia amepeleka zaidi ya sh. bil 2.9 ili kuboreshwa upatikanaji huduma ya maji safi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kibondo (KIUWASA) Mhandisi Aidan Ngatomela ,ametoa takwimu hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake hivi karibuni.

Anasema katika miaka mitatu ya utawala wa Rais Samia, hali ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama ya bomba kwa wakazi wa Mji huo imeboreshwa kwa kiasi kikubwa na kupunguza adha iliyokuwepo.

Anabainisha kuwa Rais Samia amewapelekea zaidi ya sh. bil 2.9 kwa ajili kuifanyia maboresho makubwa miundombinu ya maji na kutekelezwa miradi mipya zaidi ya sita ambayo imepelekea upatikanaji huduma ya maji kuongezeka mara dufu.

“Hali ya upatikanaji huduma ya maji katika Mji wetu wa Kibondo haikuwa shwari hata kidogo, kwani maji yalikuwa yanapatikana mara 1 au 2 kwa wiki nzima, lakini baada ya Rais kuingia madarakani amepunguza sana kilio cha wananchi,” anasema.

Mhandisi Ngatomela ameeleza kuwa kutekelezwa kwa miradi hiyo kumewezesha hali ya upatikanaji huduma ya maji katika Mji huo kuongezeka kutoka asilimia 37.1 ya awali hadi kufikia asilimia 67.6 na inaendelea kuongezeka zaidi.

Aidha idadi ya wateja wanaohudumiwa na KIUWASA imeongezeka kutoka 2,160 hadi kufikia 2,838 na uzalishaji maji umeongezeka kutoka lita za ujazo 2,108,000 kwa siku hadi lita 3,030,000 kwa siku na mtandao wa bomba umefikia km 60.

Anabainisha manufaa mengine yaliyopatikana kutokana na uwepo wa maji kuwa ni kuongeza hali ya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali, kujengwa kwa vyoo na kuboreshwa mazingira ya wafanyakazi wa kwenye vyanzo vya maji.

Mhandisi Ngatomela ametaja miradi iliyotekelezwa kuwa ni mradi wa Twabagondozi uliogharimu zaidi ya sh. mil 330 uliohusisha ujenzi wa kisima, nyumba ya mlinzi, tenki la lita 225,000 na tenki dogo la lita 50,000 na ulazaji bomba lenye urefu wa km 2.3.

Mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na kumaliza kero ya maji kwa wakazi wa Mji huo hasa wanaoishi katika Mitaa ya Malagarasi, Stendi Mpya, Maduka Saba, Kumwayi na Katunguru A, mradi huu huzalisha lita 320,000 kwa siku.

Mingine ni Mradi wa Uboreshaji Huduma ya Usambazaji Maji Kibondo Mjini awamu ya II ambao umegharimu zaidi ya sh mil 430 na mradi wa kuendeleza visima na kuchimba kisima kirefu Kibondo Mjini uliogharimu zaidi ya sh mil 145.

Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Kusafisha na Kutibu Maji ya Mto Mgoboka kwa gharama ya sh. mil 595, mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na kuongeza ubora wa maji yanayotoka katika chanzo hicho.

Mhandisi Ngatomela amebainisha miradi mingine inayoendelea kutekelezwa kwa fedha za Rais Samia kuwa ni ujenzi wa tenki la lita mil 1.5 na ulazaji bomba (sh mil 400) na Usambazaji Maji Mjini Kibondo awamu ya III (zaidi ya sh mil 600).

Mkoani Tabora amezinduliwa miradi mitatu ya maji wilayani Igunga. Ambapo miradi hiyo mitatu ni sehemu ya miradi saba yenye thamani ya shilingi Bilioni 2.3 ambayo itakwenda kuhudumia wananchi wapatao 41,951.

Akisoma taarifa ya miradi, Meneja wa RUWASA (W) Igunga Muhandisi Marwa Sebastian Muraza, amebainisha kuwa, miradi hiyo saba imekamilika kwa asilimia mia moja na tayari iko tayari kwa matumizi.

Ametoa pongezi na shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambapo kupitia wizara ya maji, wilaya ya Igunga imepata fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji.

Nao baadhi ya wananchi wanaofaidika na miradi hiyo, wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kusogeza huduma bora ya maji vijijini, na kwamba sasa watatumia muda wao katika shughuli za kiuchumi badala ya kutumia muda huo kutafuta maji umbali wa zaidi kilometa tano.

Uzinduzi wa miradi hiyo saba ni sehemu ya mIradi ya maji 57, ambayo RUWASA mkoa wa Tabora hadi kufikia mwezi Machi, 2023 itakuwa imeitekeleza, yenye thamani ya Tshs. Bilioni 61.1 ambapo miradi 46 yenye thamani ya Tshs. Bilioni 54.5 inatekelezwa na wakandarasi na miradi 11 yenye thamani ya Tshs. Bilioni 6.6inatekelezwa na wataalam wa ndani (Force Account).

Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa 2024, Mzava anaeleza, Rais Samia Suluhu Hassan amejipambanua kutoa fedha za kutosha kwenye sekta ya maji ili kusogeza huduma ya maji safi,salama .

Ametoa kauli hiyo Aprili 30 April wakati akikagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa maji , ujenzi wa tanki la maji Lita 50,000 kijiji cha Kidomole Halmashauri ya Bagamoyo Mkoani Pwani mradi ambao utagharimu milioni 176, umefikia asilimia 90 utahudumia kaya 700 zenye wakazi 3,660.

Anaeleza kwamba , mradi ni mzuri na unaridhisha ila kazi zilizobakia zikamilishwe . “Maji hayana mbadala, kila siku lazima tuguse maji ,kwa umuhimu huo Rais Samia anaendelea kuboresha miundombinu ya maji , kushusha fedha kwenye miradi ya huduma, kujenga miradi ya maji ilihali wananchi wapate huduma na maji safi ,salama yenye uhakika na karibu na mazingira ya wananchi, “anasema Mzava.

Vile vile Mzava anasisitiza, watendaji kuendelea kumsaidia Rais katika jitihada zake madhubuti za kuwaletea wananchi Maendeleo na kuinua uchumi.

Naye Mke wa Rais Mstaafu awamu ya nne Salma Kikwete, anampongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayofanya nchini na kutambulika Duniani kwa weledi wake.