Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online Songwe.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameiagiza TANROADS Mkoa wa Songwe kuhakikisha barabara zote za mkoa huo zinapitika wakati wote ikiwemo kipindi cha mvua huku akitoa rai kwa wananchi kulinda miundombinu inayowekwa na serikali.
Mhandisi Kasekenya ametoa maagizo hayo wakati wa ziara ya kukagua barabara za Wilaya ya Ileje na akaahidi kukagua miradi mingine inayoendelea katika Wilaya za Mbozi, Momba na Ileje kujionea maendeleo na utekelezaji wa kazi hizo.
Sanjari na maelekezo hayo, Mhandisi Kasekenya ameihimiza TANROADS Mkoa Songwe kuhakikisha mchakato wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Isongole-Itumba-Shigamba Ibaba-Katengere- Kafwafwa/Kimo na barabara unganishi za Katengere-Ibungu na Katengere-Isoko unaendelea haraka kwani imo katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Akiwa wilayani Ileje,Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Kasekenya, alitembelea na kukagua miradi inayosimamiwa na TANROADS wilayani humo na kujionea kasi ya utekelezaji inavyoendelea.
Utekelezaji huo umehusisha ujenzi wa barabara za zege (rigid pavement), ukataji wa milima kuondoa kona na kuimarisha miteremko (landslides) katika barabara za Isongole II Isoko kilomita 52.414, Ibungu Kafwafwa km 46, Isongole Itumba shigamba hadi Ibaba km 72 na Ndembo Ngana km 28.
Pia amekagua mradi ya ujenzi wa daraja (Box culvert) ikiwa ni matayarisho ya kuboresha mlima Mlale/Ileje katika barabara ya Ruanda Idiwili Hezya hadi Itumba km 79 ambayo imepangwa kujengwa kwa kiwango cha lami ambapo sehemu ya Ruanda Idiwili km 21 tayari zimeanza katika Wilaya ya Mbozi.
Aidha, mhandisi Kasekenya alitumia fursa hiyo kuwapongeza TANROADS Songwe kwa kusimamia vizuri miundombinu na miradi kwa ujumla.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua