Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Imeelezwa kuwa hatua za makusudi zisipo chukuliwa za kudhibiti taka za plastiki kuingia katika fukwe za maziwa na bahari itachangia kupunguza samaki ifikapo mwaka 2050.
Hii ni kutokana na tafiti zilizofanywa ambazo zinaonesha taka zitakuwa nyingi zaidi kuliko samaki hali itakayochangia kushindwa kufikia adhima ya serikali ya kuwa na uchumi wa bluu ambayo imetoa kiasi cha zaidi ya bilioni 7 kwa ajili ya kuwezesha vijana katika ufugaji wa samaki ambao unategemea maziwa na bahari.
Hayo yamebainishwa Septemba 14,2023 na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emily Kasagara,wakati akifungua kikao kazi cha kuwasilisha matokeo/mrejesho wa kampeni ya fukwe safi za maziwa makuu yenye lengo la kukusanya taarifa na takwimu za taka katika mialo ya maziwa makuu nchini iwemo Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa, kilichofanyika jijini Mwanza.
Kampeni hiyo inatekelezwa kwa kushirikiana kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SOAF-UDSM), EMEDO, Halmashauri ya Jiji la Mwanza na ARENA RECYCLING kwa ufadhili wa shirika la NORCE kutoka nchini Norway.
Kasagara ameeleza kuwa licha ya jitihada za serikali katika kudhibiti taka ngumu ikiwemo za plastiki lakini zimekuwa zikiongezeka kila mwaka kutokana na shughuli za kila siku ikiwemo kijamii,kiuchumi,usafirishaji na nakadhalika
“Tafiti zinaonesha kuwa kama hali hii itaendelea bila kudhibiti taka hizi za plastiki kuingia katika maziwa na bahari,tusipo chukua hatua za makusudi kufikia 2050 basi ndani ya ziwa na bahari tutakuwa na taka nyingi kuliko samaki hivyo uchumi wetu wa bluu utakuwa umeathiriwa,”ameeleza Kasagara.
Ameeleza kuwa serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kupiga marufuku uzalishwaji wa mifuko ya plastiki ambayo imemsaidia kupunguza tatizo na itaendelea kusimamia kupitia Wizara husika kuhakikisha taka hizo zinadhibitiwa.
Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam-Shule Kuu ya Sayansi na Teknolojia ya Uvuvi Dkt.Bahati Mayoma, ameeleza kuwa kampeni ya Fukwe Safi Maziwa Makuu lengo lake ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kudhibiti taka ngumu zinazotokana na plastiki.
“Kampeni yetu ilianza Februari 28 mwaka huu,ilizinduliwa jijini Mwanza kwa upande wa Ziwa Victoria na baadae ikaendelea kufanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Wilaya ya Nyamagana, Ukerewe,Kigoma Ujiji kwa upande wa Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa tulifanya Kyela,awamu ya kwanza ilifanyika vizuri tulikamilisha maeneo yote na kiwango cha taka kilikuwa kikubwa,awamu ya pili tulianza Agosti hadi Septemba na tukaongeza maeneo mawili mapya ya Mkoa wa Mara na Simiyu,”.
Ameeleza kuwa kiwango cha taka za plastiki ni kikubwa nchini katika vyanzo vya maji kama zilivyo nchi nyingine duniani huku chanzo kikuu ni matumizi yasiyo endelevu yanayotokana na jamii yenyewe kutozingatia taratibu zilizowekwa na serikali za kutochafua mazingira.
“Mimi pamoja na watafiti wengine mwaka 2014,2015 tulianza utafiti wa taka za plastiki na tukagundua tatizo hilo lipo nchini na mwaka 2018 serikali ilipitisha sheria ya kudhibiti matumizi yasiyo endelevu ya mifuko ya plastiki, tukaendelea kufanya tatifi nyingine 2019,2020 tukaona tatizo hili bado lipo tukaona njia rahisi kwa sisi watafiti ni kurudi kwenye jamii na kuishirikisha kuwa mabalozi wa kudhibiti taka kwani serikali pekee yake haiwezi kwani taka zinatokana na mtu mmoja mmoja ndio sababu ya kuja na hii kampeni,”ameeleza Dkt.Bahati.
Pia ameeleza kuwa katika taka walizokusanya nyingi ni chupa za plastiki zikifuatiwa na mifuko ya plastiki bahati mbaya kwa baadhi ya maeneo bado mifuko ya plastiki ambayo serikali imezuia inaendelea kuonekana ni ishara kuwa kuna wachache ambao wanakiuka taratibu ambazo serikali imeweka katika kuhakikisha inadhibiti.
Sanjari na hayo anaeleza kuwa kitu kingine walicho kibaini na kuwashangaza ni kuwa ata taka zinazotokana shughuli za uvuvi kama nyavu zilizotelekezwa na vigungashio mbalimbali vinavyotumika katika sekta hiyo vimeibuka miongoni mwa taka tano zinazopatikana kwa wingi katika kwenye maziwa kupitia kampeni hiyo.
Vilevile ameeleza kuwa tafiti duniani kote zinaonesha kuwa taka za plastiki zinaweza kuathiri viumbe hai wa majini kwa namna mbalimbali ikiwemo kuzonga samaki na kusababisha kufa pamoja na kipande cha plastiki kumezwa na samaki ambacho hakiwezi kumengenywa na kusababisha wanakufa kimya kimya hivyo ni changamoto ambayo inahitaji kushughulikia.
“Tusipochukua hatua sasa maana yake ndoto ya uchumi wa bluu ya serikali inaweza isifikiwe kwani samaki watakufa,hivyo ili kufikia adhima hiyo ambapo kile kinachofanya uchumi wa bluu iwe mazingira,samaki wenyewe,maji lazima viwe na ubora unaokubalika kimataifa na kitaifa ndio maana tunasema tuchukue hatua sasa kunusuru viumbe vyetu,” amesema Dkt Bahati.
Naye Mwanzilishi wa Arena Recycling Industry Zagaco Emanuel, ameeleza kuwa katika mradi huo wameshiriki katika kudhibiti taka ambazo zimekusanywa kutoka kwenye fukwe takribani 68 ambazo wamezifanyia usafi kutoka katika maziwa makuu matatu.
Ambapo taka ambazo siyo rejerezi wamekuwa wakizipeleka kwenye madampo na zile taka rejerezi wametafuta namna ambavyo zinakwenda kutumika.
“Tunategemea bidhaa kwa kutumia taka za plastiki ambazo ni rafiki kwa mazingira ikiwemo matofali ambayo unaweza kujenga bila kutumia saruji ambazo zinapunguza gharama za ujenzi,” amesema Emanuel.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu