Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
MDHAMINI Mkuu wa Tamasha la Kariakoo ‘Kariakoo Festival 2024,’ Benki ya NMB, imeahidi maboresho na udhamini mnono zaidi wa tamasha hilo linalofanyika kwa wiki moja katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia Jumanne ya Septemba 17 lilipofunguliwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila, ndiye aliyefungua tamasha hilo, linalowakutanisha pamoja wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo nchini ili kuuza bidhaa zao kwa bei punguzo, sambamba na kuwaunganisha na wateja wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Alex Mgeni ambaye ni Mkuu wa Idara ya Biashara ya NMB – iliyodhamini tamasha hilo kwa zaidi ya Sh. Mil. 80, aliipongeza Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Kampuni ya One Voice kwa kushirikiana na Katibu Tawala kwa wazo lililozaa tamasha hilo.
“Tukiwa kama wadau vinara wa maendeleo, tuko tayari kushirikiana na wafanyabiashara wa Kariakoo kwa sababu wao ni muhimu katika ujenzi wa Uchumi wa taifa letu, mwakani tutakuja na nguvu kubwa zaidi, maboresho makubwa na udhamini mnono zaidi.
“Kama ulivyoona kuna taasisi mbalimbali za Serikali ziko hapa, uwepo wao sio tu unatupa furaha na Faraja sisi wadhamini, bali pia unarahisisha urasimishaji wa biashara, na unaenda kumaliza changamoto mbalimbali zinazowagusa moja kwa moja wafanyabiashara wetu,” alisisitiza.
“Idara yangu inaupongeza uongozi wa NMB kwa kukubali kushiriki tamasha hili kwa kiwango hiki na kama nilivyotangulia kusema, huu ni mwanzo tu, tutaendelea kuliboresha zaidi tamasha hili hapo mwakani kwa kutanua udhamini wetu,” alisema Mgeni.
Licha ya kusisitiza kuja kivingine na maboresho ya udhamini, Mgeni alisema NMB kupitia banda lao katika tamasha hilo wanatoa huduma na elimu ya fedha, mikopo na bima kwa wananchi, na bidhaa kuu waliyoenda nayo hapo NMB Lipa Namba kwa watoa huduma wanaoshiriki.
“Sisi NMB, bidhaa kubwa tuliyokuja nayo hapa ni huduma ya Lipa Namba, katika kila banda kuna ‘sticker’ za NMB Lipa Namba, mfumo rahisi, salama na nafuu zaidi wa ulipiaji bidhaa kwa wanunuzi wanaokuja hapa ama wale wanaoagiza kupitia mtandaoni,” alisema Mgeni.
Kwa upande wake, Dk. Nguvila alikiri kuvutiwa na maono yaliyozaa tamasha hilo, na kwamba licha ya kushirikishwa mapema na kubariki uanzishwaji wake, lakini ubunifu na uwezeshaji wa NMB na Wadhamini Wenza umelipa tamasha hilo sura ya kimataifa katika mwaka wake wa kwanza tu.
“Kama alivyosema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, wazo hili halikuanguka tu, bali limetokana na ubunifu wa wafanyabiashara na wadau wa maendeleo waliotamani kufanya mapinduzi ya kibiashara katika eneo la Soko Kuu la Kariakoo.
“Mpango mkakati uliopo ni kufungua milango ya kulifanya Soko la Kariakoo na wafanyabiashara wake kuhudumia kwa masaa 24, Kariakoo Festival ni njia ya kuimarisha biashara ya kimataifa na kufanya kazi kwa siku saba za wiki kwa msaa 24,” alisema Dk. Nguvila.
Dk. Nguvila alizitaka taasisi zote muhimu za Serikali zinazofungamana na wafanyabiashara kama vile Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Shirika la Viwango Tanzanaia (TBS), Tume ya Ushindani (FCC) na Shirika la Bima la Taifa (NIC), kuhakikisha wanashiriki tamasha hilo bila kukosa.
“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameshafanya kazi yake, kama ni sera nzuri ameshaziweka, mazingira wezeshi yameimarishwa, sheria kandamizi ameziondoa, kilichobakia sasa ni kwa taasisi za Serikali yake kushirikiana na wafanyabiashara kukuza Uchumi wao na kulipa kodi,” alisema.
Awali akikaribisha wageni, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martin Mbwana, alimpongeza Dk. Nguvila kwa uharaka wa kutambua ukubwa wa wazo la Kariakoo Festival, huku kipekee akiishukuru NMB kwa kuthamini maono yao na kudhamini tamasha hilo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi