Na Mwandishi Wetu
MABEKI wa Simba SC, Shomari Kapombe Na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wameongezwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kinachojiandaa na mchezo wa marudiano wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda hapo kesho.
Kapombe na Tshabalala waliachwa katika kikosi cha Stars kilichocheza mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda uliofanyika Ismailiya nchini Misri hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Rais wa TFF Wallace Karia alisema, Kocha wa Taifa Stars Adel Amrouche amewaongeza kikosini wachezaji hao ili waweze kuisaidia timu katika mchezo wa kesho dhidi ya Uganda.
“Mwalimu amewaongeza kwenye kikosi wachezaji wetu wazoefu Shomari Kapombe na Mohamed Hussein kwa ajili ya mchezo wetu wa marudiano dhidi Uganda na tayari wachezaji hao wapo kambini.
“Maneno yalikuwa mengi sana baada ya uteuzi uliofanyika mwanzoni lakini tumeona matunda yake, kuongezwa kwa Kapombe na ‘Tshabalala’ ni pendekezo la Kocha Mkuu, Adel Amroache,” alisema Karia.
Katika hatua nyingine Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo na Afisa Habari wa Yanga SC, Ally Kamwe wamesema hatakiwi mtu kubaki nyumbani kwenye mchezo wa kesho.
Maneno ya Maofisa hao wa habari ni kwa ajili ya kuhamasisha Watanzania, kwenda katika dimba la Benjamin Mkapa kesho kuishangilia Taifa Stars kwenye mchezo dhidi ya Uganda.
Taifa Stars ilishinda mchezo wake wa kwanza ugenini dhidi ya Uganda Cranes uliochezwa Machi 24, mwaka huu katika Uwanja wa Suez Canal nchini Misri kwa bao pekee la Simon Msuva.
Stars ipo nafasi ya pili kwenye kundi F na pointi nne, nyuma ya vinara Algeria walioshinda mechi zote tatu huku Niger ikishika nafasi ya tatu na pointi mbili na Uganda ikiburuza mkia na pointi moja.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba