*Mfumo wakusanya tani milioni 1.1, wakulima walipwa trilioni 2.4
*Mfumo wakua kwa asilimia 43 msimu 2025/26
*Ajira 11,000 zapatikana kupitia maghala
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Simiyu
Serikali imesisitiza kuwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni mfumo muhimu na kichochezi kuelekea utekekalezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Huku ikiendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kunafanyika urasimishaji wa bidhaa za Tanzania kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala,ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kulinda maslahi ya wakulima, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa nchi.
Hayo yameelezwa Februari 25,2026 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga,wakati wa kufunga msimu wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala msimu wa 2025/2026 na kufungua msimu mpya wa 2026/2027,hafla iliofanyika mkoani Simiyu.

Kapinga,amesema,mfumo wa Stakabadhi za Ghala unatekelezwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,kwani mfumo huo unatoa mchango wa moja kwa moja katika kutekeleza dira hiyo.
Kupitia mfumo huo wanakuza uchumi shindani,ushindani katika soko,kukuza mapato ya wananchi na kupunguza umaskini,kuimarisha upatikanaji wa mitaji na huduma za kifedha vijijini,kuchochea mageuzi ya kilimo na biashara za mazao,kukuza viwanda na mnyororo wa thamani.
Kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, kukuza mifumo ya TEHAMA na matumizi ya kidigitali,kuimarisha nafasi ya vijana na wanawake katika uchumi,kuchangia usalama wa chakula pamoja na kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno.
“Nasisitiza kuwa msimamo wa Serikali na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na ilani ya CCM,kwamba Stakabadhi za Ghala ni ulinzi wa wakulima.Mara kadhaa Rais amekuwa akisisitiza na kuelekeza kuwa mauzo ya mazao lazima yaendane na bei ya soko na siyo shinikizo la nje ya soko halisi,mfumo lazima uzingatie haki,uwazi,kulipa kwa wakati na kuzuia ubadhilifu,”amesema Kapinga.
Sanjari na hayo Kapinga, amesema, kutokana na upanuzi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika maeneo mapya na ongezeko la mazao yanayouzwa kupitia mfumo huo, bado kumekuwepo na changamoto ya uelewa mdogo miongoni mwa wadau katika baadhi ya maeneo.
“Ninaielekeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB),kutoa elimu kwa wadau wa sekta mbalimbali na kuhakikisha mfumo unatekelezwa kwa ufanisi,”amesema Kapinga.
Pia amesisitiza kuwa mkazo uwekwe katika utoaji wa mafunzo na uhamasishaji kwa wakulima, wafanyabiashara, wasimamizi wa ghala, na wadau wengine muhimu ili kuongeza uelewa na kuboresha ushiriki wao katika mfumo huo.
Huku bodi hiyo kuhakikisha wale wenye maghala ambayo hayajakidhi vigezo,wanawezeshwa ili wafanikiwe kutoa huduma bora na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa mfumo huo.

Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala(WRRB), Asangye Bangu,amesema kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika msimu wa 2025/2026,zaidi ya tani milioni 1.1 za mazao zilikusanywa na kuuzwa ikiwa ni ongezeko la asilimia 43 ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2024/2025.
Huku wakulima wakilipwa takribani shilingi trilioni 2.4 kupitia mauzo hayo na mazao yalioongoza ni pamoja na korosho tani 439,088 asilimia 39 kwa mikoa ya Morogoro, Singida, Pwani, Lindi, Mtwara,Ruvuma, Tanga na Mbeya.
“Mbaazi tani 270,739 sawa na asilimia 25 kwa mikoa ya Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma,Manyara, Katavi, Rukwa,ufuta tani 221,603 sawa na asilimia 19 kwa mikoa ya Morogoro, Pwani, Lindi, Ruvuma, Iringa, Songwe,
Katavi, Rukwa,”amesema.
Amesema mbali na hayo pia ajira rasmi 1,430 zilipatikana katika maghala huku zaidi ya ajira 10,000 zisizo rasmi zilipatikana na kwa sehemu kubwa ni vijana huku halmashauri zilipata takribani shilingi bilioni 65 kama ushuru.
“Ghala 286 zilipatiwa leseni ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 kutokana na kutanuka kwa matumizi ya mfumo,idadi ya waweka mali iliongezeka kutoka 224 hadi 788 sawa na ongezeko la asilimia 25,hii ni
kutokana na mikoa ya Kanda Ziwa kutekeleza mfumo huo. Wilaya zinazotumia mfumo zimeongezeka kutoka 65 msimu wa 2024/2025
hadi 114 2025/2026,”amesema.
Pia amesema,kuna changamoto ya uhaba wa maghala bora hivyo wanahimiza sekta binafsi na Halmashauri kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya kisasa huku bodi hiyo imejipanga kuanza matumizi ya ghala
zianazo hamishika ili kusaidia maeneo yenye uhaba wa miundombinu ya ghala
Sanjari na hayo amesema,katika msimu wa 2026/2027,bodi hiyo itaweka mkazo katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA kupitia mfumo wa WRS-MIS,kupanua matumizi ya Meneja Dhamana katika bidhaa ya nafaka na mafuta.
Pia kuratibu rasmi ushiriki wa sekta ya mifugo, ngozi na mwani pamoja na kutoa elimu kwa wakulima, vyama vya ushirika na wakusanyaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Anamringi Macha,amesema kufunga na kufungua msimu wa mauzo ya mazao katika Mkoa huo kumekuwa chachu na hamasa kwa wananchi kwani kwameelewa maana na faida za kuendelea kutumia mfumo huo.
Nao mmoja wa wakulima wa Mkoa wa Simiyu,Mariam Litwina, amesema,wakulima wananufaika na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala,kwa kuuza mazao yao katika mnada kwa uwazi kwa bei nzuri na kupata fedha kwa wakati.
Huku wafanyabiashara mkoani Simiyu akiwemo,Daud Mpina,amesema kupitia mfumo huo wanapata soko la uhakika na wateja kutoka nje ya Mkoa huo kwa urahisi huku akiiomba Serikali kuendelea kuboresha mfumo huo.




More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama