February 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga: PURA endeleeni kuwavutia wawekezaji utafutaji Mafuta, Gesi

*Ataka Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kuwa na matokeo chanya

*Aipongeza PURA kuwashirikisha Watumishi kujadili mipango ya Bajeti ya Taasisi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), kuendelea kuvutia uwekezaji katika vitalu vilivyo wazi vya mafuta na gesi asilia ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini.

MKapenga ameyasema hayo leo wilaya ya Morogoro, Mkoani Morogoro, wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa PURA kinacholenga kujadili masuala mbalimbali ukiwemo mpango na Bajeti ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) Mhandisi. Charles Sangweni (kushoto). Kulia ni Katibu wa Baraza Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA) Ebeneza Mollel,wakati wa Kikao cha Baraza hilo cha kujadili Mpango na Bajeti hilo linalofanyika tarehe 18 na 19 Februari 2025, mkoani Morogoro.

“Mkifanikiwa kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi, nchi itaongeza ugunduzi wa rasilimali hiyo muhimu ikiwa ni pamoja na kuogeza futi za ujazo wa gesi inayopatikana nchini.

“Pia, mkiendelea kuvutia uwekezaji kupitia Duru ya Tano ya kunadi vitalu itakayozinduliwa mwezi machi mwaka huu, pamoja na faida zilizopo, mtakuwa mmeendeleza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuifungua Tanzania kiuchumi na kuvutia uwekezaji zaidi,”amesema Kapinga.

Amesema, Wizara ya Nishati inatambua umuhimu wa tukio la Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini pamoja na kutambua kazi kubwa ambayo imeshafanyika kuelekea uzinduzi wa tukio hilo, ambapo amesema ni muhimu katika
kuvutia uwekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

“Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukizungumzia ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 57.54 pekee ni wakati sasa wa kufanya zaidi na zaidi ili tuweze kuongeza ugunduzi wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa,” amesisitiza Kapinga.

Katika kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi, ameupongeza uongozi wa PURA kwa kuendelea kuwashirikisha watumishi wake katika kujadili, kupanga na kupitisha mipango na Bajeti ya Taasisi kwenye Baraza la Wafanyakazi ikiwa ni utekelezaji pia wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) wakati wa Kikao cha Baraza hilo linalofanyika tarehe 18 na 19 Februari 2025, mkoani Morogoro. Kushoto Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) Mhandisi. Charles Sangweni.

Amesema, kufanyika kwa vikao hivyo ni ishara tosha ya utawala bora mahala pa kazi kwa kuwa watumishi wanapata fursa ya kuchangia mawazo yao kuhusu hali ya uendeshaji wa Taasisi hivyo kuendelea kuwa ni sehemu muhimu ya Taasisi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA), Mhandisi. Charles Sangweni amesema duru ya tano (5) ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na
gesi asilia nchini inatarajiwa kuzinduliwa mwezi Machi, 2025 Jijini Dares salaam, wakati wa Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki (EAPCE’25).

Amesema, PURA inaendelea kusimamia na kudhibiti shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia katika vitalu mbalimbali nchini na Kuhakikisha watanzania wazawa wanashirikishwa katika miradi mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli nchini.