March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga na matarajio ya kuleta matokeo kufikia maono  ya Rais Dkt.Samia

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI  wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema dhamira ya serikali ya awamu ya sita katika kukuza viwanda imeonyesha mafanikio  katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan huku akiahidi kuilinda imani aliyopewa yakusimamia wizara hiyo kwa kuhakikisha matarajio na maono ya Rais na wananchi yanafanikiwa. 

Akizungumza jijini Dodoma  wakati wa makabidhiano ya ofisi Novemba 20,2025 ,Kapinga amesema hana mashaka na watumishi wa Wizara hiyo kwani anaamini watampa ushirikiano kufikia malengo ya kuhakikisha watanzania wanapata matokeo kupitia utumiahi wao .

“Naamini wote tupo kwa ajili ya kuhakikisha watanzania wanapata matokeo,tushirikiane kwa umoja wetu kufikia maono hayo ya Rais wetu Dkt.Samia.”amesisitiza Kapinga

Kwa upande wake, Waziri wa Wizara hiyo aliyemaliza muda wake  Dkt.Selemani Jafo amesema wizara imepata  viongozi wapya ambao anaamini ni watu sahihi watakaosukuma mbele masuala ya sera, maendeleo ya viwanda na uwekezaji. 

Aidha Dkt.Jafo ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt.Samia kwa kumwamini kwa kipindi chote alichohudumu katika Wizara hiyo.

Naye Naibu Waziri, Patrobasi Katambi, ametoa wito kwa watumishi wa wizara kuongeza ushirikiano, akisisitiza kuwa uongozi utaendelea kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza ufanisi.