Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, ametoa wito kwa wananchi na wabunge nchini, kutembelea Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, ili kufahamu masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Naibu Waziri Kapinga ametoa wito huo, leo Aprili 15, 2024 baada ya kutembelea mabanda ya Maonesho hayo na kujionea jinsi Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Wadau wake walivyojipanga tayari kwa kuhudumia wabunge na wananchi watakaotembelea maonesho husika.
“ Nawakaribisha wananchi na wabunge kwenye wiki hii muhimu sana ya Nishati, ambapo tunaonesha kazi mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake, tunatatua kero mbalimbali zinazowasilishwa na pia wabunge na wananchi watajionea utekelezaji wa miradi katika wilaya zote, majimbo yote na mikoa yote Tanzania.” Amesema Kapinga.
Ameongeza kuwa, katika Maonesho hayo taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na kampuni zake tanzu zimeshiriki.
Kapinga amesema kuwa, katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kazi kubwa imefanyika katika Sekta ya Nishati akitolea mfano utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao umeshaanza kuzalisha umeme, miradi ya usambazaji umeme mijini, vijijini na vitongojini, nishati safi ya kupikia pamoja na sekta ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia.
Aidha, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Kapinga amemshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson kwa kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Nishati ambao umewezesha Wiki ya Nishati kufanyika kwa umahiri mkubwa.
Maonesho ya Wiki ya Nishati yaliyoanza leo yatahitimishwa tarehe 19 Aprili 2024 ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko atayafungua rasmi tarehe 16 Aprili 2024.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu