Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Kwimba
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amezitaka Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kuimarisha utekelezaji wa majukumu yao kuanzia ngazi ya mkulima shambani hadi sokoni badala ya kuanzia ghalani pekee.
Ili kuleta tija na ufanisi wa zao la choroko kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala,ambao ameeleza kuwa msaada kwa wakulima katika kupata soko la uhakika na bei nzuri.

Kapinga alitoa kauli hiyo Februari 25, 2026, baada ya kushuhudia mnada wa uuzaji wa zao la choroko uliofanyika katika ghala teule la mfumo wa stakabadhi za ghala la Ndilima Warehouse, Kata ya Hungumalwa, wilayani Kwimba, mkoani Mwanza.
Alisema mfumo wa stakabadhi za ghala haupaswi kuanza wakati mazao yanapoingia ghalani, mpaka bali unapaswa kuanzia shambani kwa kumsaidia mkulima kuzalisha mazao bora, kuyakusanya kwa ubora na hatimaye kutafuta bei nzuri kupitia minada.
“Wengi wanaamini mfumo wa stakabadhi za ghala unaanzia ghalani, lakini maono ya mfumo huu ni kuanzia shambani. Hapo ndipo tunaimarisha uwiano wa uzalishaji hadi sokoni,” alisema Kapinga.
Alieleza kuwa COPRA tayari imeanza utekelezaji mkoani Mwanza kwa kusambaza tani 1.5 za mbegu ya choroko ingawa mahitaji bado ni makubwa.Na kwa mujibu wake Mkoa wa Mwanza unahitaji tani 20 za mbegu huku Wilaya ya Kwimba pekee ikihitaji tani tano.
“Bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Mazao bora siyo miujiza bali ni uwekezaji kwenye pembejeo, mbegu na huduma za ugani. Tutachakata kupitia taasisi zetu kuona namna bora ya kuboresha mfumo huu ili uwe na tija kwa mkulima kuanzia shambani,”alisema Kapinga.
Kapinga alisema anafarijika na mafanikio yanayoonekana katika mnada wa choroko Kwimba, akibainisha kuwa licha ya changamoto zilizopo, mwenendo wa bei unaonesha kupanda.
“Tulianza muda si mrefu kutumia mfumo huu lakini tunaona mafanikio. Mwaka jana bei ya juu ya choroko ilikuwa shilingi 1,200 kwa kilo, sasa imefikia shilingi 1,600. Hii inaonesha grafu inapanda,”alisema Kapinga.
Aliongeza kuwa maelekezo hayo yanatekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), yaliyoahidi kuimarisha na kulinda mfumo wa stakabadhi za ghala kwa manufaa ya mkulima na mfanyabiashara.
Alisema Serikali haitakuwa mdhibiti pekee bali pia mwezeshaji, hasa katika kusaidia upatikanaji wa teknolojia za kisasa maghalani ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kufikishwa sokoni.
“Teknolojia ni ghali,tukisubiri wahusika wajinunulie wenyewe itachukua muda, wakati biashara haisubiri. Ni lazima taasisi zetu zisiwe wadhibiti pekee bali na wawezeshaji kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanapata teknolojia husika kwa wepesi na haraka,”.

Alisisitiza kuwa matumizi ya mfumo wa stakabadhi za ghala si hiari na kuonya dhidi ya vitendo vya utoroshaji wa mazao, akibainisha kuwa takribani tani 95,000, ziliwahi kutoroshwa, hali isiyokubalika.
“Kwa jina lolote au lugha ya kulainisha, kutafuta masoko nje ya mfumo ni kutorosha mazao. Lazima wote tutumie mfumo huu na changamoto zitakazojitokeza zitatatuliwa ndani ya mfumo,”alisema.
Mkurugenzi wa WRRB, Asangye Bangu, alisema utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala katika eneo la Kwimba na Kanda ya Ziwa ni hatua kubwa ya mabadiliko, kwani kwa miaka mitano iliyopita mfumo huo ulikuwa ukitekelezwa zaidi mkoani Morogoro.
Alisema urasimishaji wa biashara ya mazao utasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za bei na kuondoa mianya ya wachache kunufaika kwa taarifa huku wengi wakikosa.
“Utaratibu huu unamsaidia mwananchi kujua bei halisi ya mazao yake na kupata stahiki yake kwa wakati. Tunaomba ushirika uendelee kutoa elimu na kuweka mazingira rafiki kwa mkulima kupata fedha kwa wakati,”alisema Bangu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kwimba,Ng’wilabuzu Ludigija,alisema mfumo wa stakabadhi za ghala umesaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao na kurahisisha upatikanaji wa soko. Ameeleza kuwa wilaya itakuwa na vikao viwili kila mwaka kutathmini mafanikio na changamoto za mfumo huo.
Mbunge wa Jimbo la Sumve Moses Bujaga,alisema zao la choroko kwa sasa limekuwa la kibiashara mbadala wa zao la pamba kwa wakazi wa jimbo hilo hivyo ameomba kuangaliwa kwa tozo zisizo za lazima ili kuongeza tija kwa mkulima.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kwimba,Cosmas Bulala,alisema Hungumalwa ni mji wa kibiashara na asilimia 95 ya wakazi wa wilaya hiyo ni wakulima. Amebainisha kuwa choroko hulimwa Novemba na kuvunwa Februari, huku dengu likilimwa Aprili na kuvunwa Agosti.
Hivyo aliiomba WRRB,COPRA na taasisi zingine kushiriki kikamilifu katika hatua ya uzalishaji badala ya kusubiri mavuno pekee.
“Tunapoingia shambani hatuoni mamlaka husika, lakini wakati wa mavuno ndipo wanakuja na miongozo ya bei. Tunahitaji ushiriki wao tangu mwanzo ili tuondokane na kilimo cha kubahatisha,”alisema Bulala.
Kwa ujumla, Serikali imewataka wakulima wa choroko kuendelea kuunga mkono mfumo wa stakabadhi za ghala, ikiahidi kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, mbegu na masoko ya uhakika ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.



More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama