December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kanisa la TAG Kitete lapongezwa kwa kusaidia jamii

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

KANISA la Tanzania Assemblies of God (TAG) tawi la Kitete Christian Center (KCC)x  lililopo mjini Tabora limepongezwa kwa kujitoa kwake kiroho na kimwili kusaidia jamii inayowazunguka ili kuokoa maisha yao.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mkurugenzi wa Chuo Cha Tabora Polytechnique (TPC) kilichoko mjini hapa Shaban Mrutu alipokuwa akizungumza na waumini wa kanisa hilo kwenye hafla ya uzinduzi wa albamu ya Utamaduni wa Mbinguni.

Alisema kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kijamii ikiwemo kusomesha waumini wao wanaohitaji elimu ya kumtumikia Mungu na kusaidia jamii.

Mrutu alipongeza maono makubwa ya kanisa hilo ikiwemo uamuzi wake wa kuanza ujenzi wa kanisa kubwa litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia waumini zaidi ya milioni 1.25 kwa wakati mmoja kwenye ibada au mikutano ya ndani.

‘Kwa umoja na mshikamano mlionao wana KCC, naamini kabisa mradi wenu huu wa ujenzi wa kanisa hautakwama hata kidogo, endeleeni kushikamana na kujitolea hivi hivi ili kufanikisha malengo yenu’, alisema.

Aidha Mrutu alimpongeza Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Rev.Paul Meivukie ambaye ni Askofu Mstaafu wa Kanisa la TAG Jimbo la Tabora kwa kuliongoza vizuri kanisa hilo na kubainisha kuwa maono yake ni hazina kubwa ya maendeleo.

Alitoa wito kwa waumini na kanisa zima kuendelea kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan na taifa kwa ujumla ili kudumishwa amani, utulivu na maendeleo makubwa ya wananchi.

Katika harambee ya uzinduzi wa albamu hiyo iliyoongozwa na Mgeni rasmi Mrutu jumla ya sh mil 14 ikiwemo fedha taslimu sh mil 4 zilipatikana na kukabidhiwa Mwenyekiti wa Kwaya hiyo Yona Mbeke.

Awali Rev. Meivukie alimweleza mgeni wake kuwa kwaya hiyo ni ya Kitaifa kwani imekuwa ikishiriki matukio mbalimbali yaliyobeba agenda za Kitaifa na hata mwaka huu imealikwa kushiriki maadhimisho yatakayofanyika hivi karibuni Jijini DSM ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Malawi Dkt Chakwela.

Naye Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa Tabora Ramadhan Kapela aliyeambatana na mgeni rasmi alisema madhehebu ya dini yana mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi kwani yamekuwa mstari wa mbele kuomba amani na utulivu wa nchi na huo ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote lile.

Aliahidi kuwa wataendelea kuunga mkono shughuli zinazofanywa na kanisa hilo ili liendelee kupiga hatua kubwa za kumtumikia Mungu na kusaidia jamii.

Askofu Mstaafu wa Kanisa la TAG Kitete Christian Centre lililopo mjini Tabora Rev Paul Meivukie akifungua hafla ya uzinduzi wa album ya kwaya ya Uamsho iitwayo UTAMADUNI wa Mbinguni.
Kwaya ya Uamsho ya Kanisa la TAG Kitete ikiwa imevalia nadhifu kwenye harambee yao ya uzinduzi wa album yao iitwayo UTAMADUNI wa Mbinguni….iliyofanyika juzi katika ukumbi wa Kanisa hilo lililopo mjini Tabora
Mkurugenzi wa Chuo cha Tabora Polytechnique Bw. Shaban Mrutu aliyekuwa MGENI rasmi ktk harambee ya uzinduzi wa album ya kwaya ya Uamsho iitwayo UTAMADUNI wa mbinguni iliyofanyika katika Kanisa la TAG Kitete mjini Tabora…