November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly lamtunuku tuzo Magufuli

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dodoma

UONGOZI wa Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly, kupitia Kamati Kuu na Halmashauri Kuu imemtunukia tuzo ya uongozi Rais Dkt. John Magufuli baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wake, ambapo Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.

Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Magufuli jana kwenye ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly, Baba Askofu Dkt. Yohana Masinga iliyofanyika katika makao makuu ya kanisa hilo Area C Wajenzi jijini Dodoma.

Baada ya kupokea tuzo hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na Rais mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu na katika hotuba na maelekezo yake kwa viongozi na watendaji wa Serikali amekuwa akisisitiza suala la kumtanguliza Mungu mbele katika kuwahudumia wananchi.

“Ama kwa hakika hofu ya Mungu aliyonayo kiongozi wetu ndiyo hasa siri ya kufanikiwa kwa uongozi wake na Taifa letu kwa ujumla. Sote ni mashuhuda kwamba Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa nchi ya mfano Afrika na Dunia kwa ujumla katika kupiga vita rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma sambamba na kurejesha nidhamu ya kazi ambayo ilikuwa imepotea katika ofisi za umma.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea tuzo kutoka kwa Askofu Mkuu wa kanisa la Philadephia Gospal Assemblies Dkt. Yohana Simon Masinga kwa ajili ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua uongozi wake uliotukuka katika kuwatumikia watanzania, wakati wa hafla ya kusimikwa kwa askofu mkuu wa kanisa la Philadephia Gospal Assemblies, Jijini Dodoma Desemba 20, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha hivi karibuni dunia nzima imeshuhudia jinsi Tanzania ilivyomtanguliza Mungu wakati wa mlipuko wa Homa Kali ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID19).

“Tanzania hatukujifungia ndani kama mataifa mengine. Tuliendelea na shughuli zetu kwa imani kabisa tukijua yupo Mungu ambaye ndiye kinga na msaada wetu pekee,”amesema.