November 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kanisa la Anglican kuendelea kutoa mafundisho kuzuia mmomonyoko wa maadili

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Kanisa la Anglican limesema litaendelea kutoa mafundisho ili kuzuia mmomonyoko wa maadili ambao kwa sasa umeshamiri nchini unao changia kuwa na vitendo visivyofaa ikiwemo ubakaji na ulawiti wa watoto huku jamii ikipoteza hofu ya Mungu.

Huku jamii ikihimizwa kuwapeleka watoto shule hasa wa kike na kuacha kuwaingiza katika ndoa za utotoni kwani kitendo hicho kinaelezwa kuwa ni kuwafanyia ukatili.

Akizungumza Mei 5,2024 na Timesmajira Online mara baada ya kuhitimisha harambee ya ununuzi wa gari la kanisa la Anglicana la Mtakatifu Andrea Parishi ya Igoma Mwanza ulionda sambamba na uzinduzi wa gari hilo,Askofu wa Dayosisi ya Victoria Nyanza wa kabisa hilo(DVN), Zephania Ntuza, ameeleza kuwa kama kanisa wamekuwa wakiendelea kutoa mafundisho ili watu wasimamie imara na vitendo hivyo viweze kupungua na wanaendelea kumuomba Mungu sababu kizazi hiki kina changamoto zake.

“Kumekuwa na suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii na sisi kama kanisa tunaendelea kuwafundisha kwani hivi karibuni kumekuwa na watu wanaojihusisha kimapenzi na ndugu zao,ushoga na ulawiti hivi vyote ni vitendo visivyofaa hata mbele za Mungu, viongozi wa kanisa,maaskofu na wachungaji tunafundisha injili imara ili kuweza kunusuru taifa letu kutokana na vitendo viovu kama neno la Mungu linavyosema na havimpendezi yeye,”ameeleza Askofu Ntuza.

Akizungumzia suala la utoaji Askofu Ntuza ameeleza kuwa waumini katika taasisi yao mara nyingi wamekuwa wakijitoa kwa kazi ya Mungu kutokana na kuona fedha wanazotoa zikiwa zinafanya shughuli zinazotakiwa.

“Leo tumekuwa na uzinduzi wa gari ambalo walichanga michango yao,muumini anapotoa sadaka yake na ukaenda kwenye mambo ambayo yamelengwa kufanyika wanakuwa na moyo na wanavyomtolea Mungu ndivyo wanavyobarikiwa hivyo tunashuhudia wakiinuliwa kutokana na ahadi kama ilivyosemwa kwenye maandiko kuwa ukimtolea anakubariki,”amesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa kanisa la Anglican Dayosisi ya Victoria Nyanza(DVN), Mchungaji Canon Mlugu,ameeleza kuwa
Naendelea kuwasihi vijana kwani duniani ya sasa imeharibika kuna mafundisho mengi katika mitandao ya Facebook, Twitter na mitandao mingine yote mazuri na mengine ni mabaya ambayo yanawafanya kuingia katika shida.

Hivyo amewasihi wananchi wote wa Tanzania na waumini wote kutowaingiza watoto wa kike wenye umri mdogo kwenye ndoa za utotoni kwani zinawakatisha masomo yao na kuwakatili kihisia kwa sababu hawajafikia umri huo inafika mahali wanaingia katika shida na kupoteza nguvu kazi ya kanisa na taifa kwa ujumla.

“Wazazi tuwapeleke watoto shule na tuendelee kuwahudumia mpaka pale watakapomaliza masomo na mpaka watakapifikia umri unaofaa wa kuingia katika hatua ya ndoa lakini kuingia katika ndoa utotoni ni ukatili kwa watoto,”ameeleza Mchungaji Mlugu na kuongeza kuwa

“Niendelee kuwasihi yale makabila ambayo bado yana tabia ya ukeketeji kwa watoto wa kike siyo nzuri kwani inasababisha vifo kwa kupoteza damu nyingi pia siyo taratibu ya kiMungu hivyo waache ili waweze kufuata maadili ya Mungu,”.

Hata hivyo amewaombe vijana wampende Mungu waende kanisani,wafanye kazi wasikae bila kazi kwani wakifanya kazi ndipo watapata mahitaji yao na kuona namna ya kumtumikia Mungu katika utoaji.

“Tunapo mtolea Mungu kwa njia ya sadaka ni ishara moja ya kuonesha upendo kwa Mungu ili tuweze kubarikiwa na kufanya kazi ya Mungu kama kujenga makanisa pamoja na kuhubiri injili ambayo ina gharama zake,hata kipindi cha Yesu kuna watu waliokuwa wanatoa sadaka ili kazi ya Mungu iende mbele,kama waumini tunapaswa kujitoa kwa ajili ya kazi yake,hivyo nawashukuru waumini wa Igoma kwa kujitoa na kuweza kununua gari ya kanisa ambalo litasaidia kueneza injili,kuwafikia wajane,waumini kwa ajili ya kuwaombea pamoja na shughuli zote za kikanisa,”ameeleza.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Maendeleo wa kanisa la Anglican la Mtakatifu Andrea Parishi ya Igoma George Mhina, ameeleza kuwa lengo la harambee ya kuhitimisha ununuzi wa gari ya kanisa ni kuboresha huduma ya Mungu hasa katika kupeleka neno la Mungu kwa watu wengi zaidi sasa hivi tunaona imani imeanza kupunguza kwa watu wengi na matukio mengi ya ukatili na ubakaji yamekuwa yakiongezeka.

Ambapo ameeleza kuwa chanzo cha vitendo hivyo ni vijana kutolelewa katika maadili ya dini hivyo gari hilo litakuwa ni sehemu moja wapo ya kufikia watu wengi zaidi ili wapate elimu ya dini na kuweza kuwakuza vijana katika maadili ya Mungu.

Naye mmoja wa waumini wa kabisa hilo Christiana Machaka ameeleza kuwa kama muumini anaamini katika kumtolea Mungu kuna faida nyingi ambazo watu wanazipata binafsi ameisha ona vitu vingi Mungu amtendea kupitia utoaji.

“Gari hilo litasaidia vitu vingi katika jamii kwani Mchungaji na viongozi wengine watapata nafasi kwa ajili ya kuhamasisha injili pia katika kusisitiza maadili katika jamii zetu kwa sababu hivi sasa kuna mambo mengi ambayo yanatokea katika jamii hususani ukatili,”.

Pia ameeleza kuwa kama mama na mkristu ana nafasi kubwa ya kuchangia maadili katika familia kwa kuwaeleza watoto na kuwafundisha wakiwa wadogo nafasi yao katika familia,kanisa na jamii ili kuondokana na matatizo ambayo yanaendelea kujitokeza katika jamii.

“Chanzo cha yote ni watoto wengi kukosa muda wa kukaa na familia kwa sababu wazazi wengi tumekuwa ‘bize’ na mambo yetu kuliko kukaa na kuwaeleza watoto wetu misingi ya Kiimani,kimaadili hata wakiwa wakubwa inaweza kusababisha pia mmomonyoko wa maadili na kusababisha vitendo vya kikatili vinavyoendelea katika jamii,”.

Mhandisi Nyerere Lucas, ameeleza kuwa imekuwa ni shida kubwa ya mmomonyoko wa maadili katika jamii hivyo muda umefika kuachana na tabia hizo na kuwa na hofu ya Mungu.

Huku akisisitiza kuwa kutoa kwa Mungu huwezi kifilisika hivyo ukipata ata kidogo mtolee Mungu moja ya kumi na utapata baraka.