Judith Ferdinand,Timesmajira Online-Mwanza
Wananchi na wafanyabiashara wa Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela mkoani Mwanza,wamehimizwa kuendelea kufanya usafi wa mazingira kila wakati badala ya kusubilia siku maalumu.
Wito huo umetolewa Februari 28,2026 na Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abdulrahman Kange,wakati wa zoezi la ufanyaji usafi wa mazingira katika soko la Msuka, lililopo ndani ya kata hiyo ikiwa ni utekelezaji wa usafi wa mwisho wa mwezi.

Kange amesema,wafanyabiashara na wananchi wa Kata ya Nyamanoro wamejitokeza kushiriki zoezi la usafi kwa lengo la kuhakikisha mazingira ya soko hilo yanakuwa safi na salama kwa wauzaji na wateja wao.
“Nitoe wito kwa wananchi kuendelea kudumisha utamaduni wa usafi si kwa siku maalum tu, bali iwe sehemu ya maisha yao ya kila siku.Mazingira safi ni msingi wa afya bora na maendeleo ya jamii,”amesema Kange.
Pia amesema,katika kuunga mkono juhudi za usafi wa mazingira sokoni humo, ametoa vifaa vya kutunzia taka taka(dustbin) kwa wafanyabiashara wa soko hilo,hatua inayolenga kuimarisha usimamizi na kuzuia uchafuzi wa mazingira.
Sanjari na hayo Kange,amesema jiografia ya Kata hiyo kwa sehemu kubwa ni milima,hali ambayo inaweza kuwa changamoto katika usimamizi wa mazingira.
“Tumekuja na mpango wa kuwashirikisha wananchi moja kwa moja kupitia mikutano yetu ya mitaa,ambapo tiratoa elimu kuhusu usafi na umuhimu wa kutunza mazingira.Lengo ni kuweza kuepuka magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu,”amesema Kange.

Kwa upande wake mwananchi wa Kata ya Nyamanoro, Mwanabuyela Abel,amesema,ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha mazingira yanayozunguka kuwa safi.
Huku akiwahimiza wananchi wenzie hususani wa maeneo ya milima kuacha tabia ya kutupa taka ovyo na badala yake watunze kwenye mifuko au vifaa kwa kutunzia taka.
“Tusubili wanaokusanya taka wakipita ndio tupeleke taka hizo kwenye gari na siyo kama baadhi wanavyofanya,unakuta mtu anatupa taka barabarani wakati mwingine zikiwa na kinyesi hata hawajali wengine,”amesema Mwanabuyela.
Akizungumza kwa njia ya simu Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza,Dkt.Jesca Lebba,amewataka wananchi kufuata,sheria na taratibu za afya,usafi wa mazingira na mwili binafsi,kuchukua tahadhari zote na kubadilisha mfumo wa maisha pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.



More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria