Na Reuben Kagaruki, Timesmajiraonline Dodoma
KANDA ya Dodoma ni moja ya kanda 10 za Bohari ya Dawa (MSD) ikihudumia mikoa miwili, ambayo ni Dodoma na Singida na Halmashauri moja ya Kiteto, mkoani Manyara.
Kama zilizovyo kwa kanda nyingine za MSD, Kanda ya MSD Dodoma nayo ina majukumu mawili, ambayo ni kutunza na kusambaza bidhaa za afya za mteja hadi mlangoni.
Majukumu hayo katika Kanda ya Dodoma yanatekelezwa na wafanyakazi takriban 42 na magari ya usambazaji 16 wakitoa huduma katika eneo lenye square meter 5,600.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea Kanda za Iringa na Dodoma ili kujionea MSD inavyotekeleza majukumu yake hivi karibu, Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Dodoma, Juliana Mbogo, anasema Kanda ya Dodoma, inasambazaji wa bidhaa za afya katika halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma, halmashauri saba za Mkoa wa Singida na Halmashauri moja ya Kiteto, mkoani Manyara.
Naye Meneja wa Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, anasema wanafanya usambazaji bidhaa za afya hadi mlangoni kwa mteja moja kwa moja, ambapo wanaenda mara sita kwa mwaka, ambapo kila baada ya miezi miwili wanasambaza dawa.
Anasema kila mwezi wanahudumia kundi moja, ambapo katika usambazaji bidhaa za afya, Kanda ya Dodoma kama zilizovyo kwa kanda zingine, imegawa wateja wake katika makundi maiwli, kundi A na B.
Kwa Dodoma, anasema kundi A ni la wateja wa Halmashauri za Singida na kundi B ni wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma ikiwemo moja ya Kiteto.
Anasema awali walikuwa wanasambaza bidhaa za afya mara tatu kwa mwaka, ambapo walikuwa na wateja 600. Kwa mujibu wa Jumaa MSD ilipofanya maboresho na kuanza kusambaza bidhaa za afya mara sita kwa mwaka, katika Kanda yao ya Dodoma wateja wameongezeka, ambapo sasa ni zaidi ya 740.
Aidha, wanatarajia mwaka huu wanaweza kuanza kutoa huduma Wilaya ya Gairo kwa sababu ipo karibu sana na Dodoma kuliko Dar es Salaa, hivyo wanatarajia kuwa na wateja wengi zaidi.
Meneja huyo anasema MSD katika kuboresha huduma zake, sasa hivi wana huduma ambazo zimeondolewa kufanyika makao makao na zitakuwa zinafanyika moja kwa moja kwenye kanda kutegemeana na madaraka ambayo wamekaimishwa kwa mameneja wa kanda.
“Kwa hiyo kuanzia Julai (Mwezi huu) utekelezaji wa mambo yote ambayo yameng’atuliwa kutoka makao makuu tutaanza kuyafanya,” anasema Jumaa.
Anapoulizwa ni maeneo gani magumu kufikika katika kanda yake wakati wa usambazaji wabidhaa za afya, Jumaa anasema kituo kilicho karibu zaidi kiko takribani kilometa saba na kituo ambacho kipo umbali mrefu zaidi kipo Mkoa wa Singida Halmashauri ya Itigi umbali wa zaidi ya kilometa 300
“Kituo hicho ndicho kiko mbali na mazingira magumu kufikika. Lakini pia huwa tuna maeneo magumu kidogo ambayo yapo Halmashauri ya Mpwapwa, ambalo ni eneo lenye milima,” anasema Jumaa na kuongeza;
“Lakini pia huwa tunapata changamoto wakati wa masika, ambapo maeneo mengi ya Dodoma na Singida ni tambalale, kwa hiyo kuna changamoto ya kukuta barabara zimehama kutokana na maji kuwa mengi kwenye maeneo husika.”
Changamoto nyingine kwa mujibu wa Jumaa ni kunasa kwa magari wakati wa usabazaji bidhaa za afya. Kuhusu utaratibu wa kufikisha bidhaa za afya kwa mhitaji (kituo) anasema kwa bidhaa za afya ambazo ni dharura mteja anaweza kuzipata ndani ya siku mbili na hata kwa siku moja kutegemea umbali ambao mteja alipo na dharura husika.
Anafafanua kwamba kwa usambazaji wa sasa ambao wanakwenda mara sita, anasema ndani ya siku 10 tangu ‘oda’ ya mteja inafikishiwa bidhaa za afya mlangoni kwake.
Kwa mujibu wa Jumaa mfumo wa MSD unavyofanyakazi kuanzia tarehe moja ya mwezi hadi tano, ambapo wateja wanaanza kuandaa mahitaji yao na kuyafikisha ngazi ya halmashauri na kuanzia tarehe 5 hadi 10 yanakuwa ngazi ya mkoa kwa ajili ya kuidhinishwa ili oda iweze kufika kwao.
“Kwa hiyo MSD kuanzia tarehe 10 hadi tarehe ya mwisho ya mwezi husika tunatakiwa tuwe tumefikisha mzigo (bidhaa za afya).
Kwa hiyo mteja anayewahi kufikisha oda, ndiye anayewahi kupata huduma, ndani ya siku 10 mteja anakuwa amepata mahitaji yake,” anasema.
Akieleza utaratibu wa kufikisha dawa kwa mteja, Jumaa anasema zimekuwa zikifikishwa mlangoni na mfumo ambao unatumika tangu kuagiza oda ya bidhaa za afya hadi kukabidhiana unakuwa ni wa kielektroniki.
Anafafanua kuwa dawa zikifikishwa kituoni zinakabidhiwa mbele ya Kamati ya Afya na kisha kusainiwa na mpokeaji katika kituo husika, ambapo yeye kama meneja wa kanda anaweza kuangalia kwenye mfumo ni nani amepokea mzigo katika kituo husika na amepokea wakati gani.
“Kwa hiyo bidhaa za afya zinaagizwa kielektroniki na kukabidhiwa kielektroniki,” anasema Jumaa.
Aidha, anasema katika kurahisisha huduma zao, MSD imeanzisha mfumo unaojulikana kama MSD Customer Portal ambao unapatikana kiganjani (kwenye simu ya kijangani) ambapo mteja anaweza kujua ni bidhaa gani za afya zilizopo kwenye kanda zote 10 MSD akiwa kule kule aliko.
“Anaweza kujua bei ya kila bidhaa na anajua ana fedha kiasi gani kwenye akaunti yake, kwani wateja wetu wote wana akaunti zao kupitia akaunti za MSD,” anasema Jumaa na kuongeza;
“Wanaweza kujua ana akiba kiasi gani kabla hajaanza kuagiza bidhaa za afya. Kwa hiyo baada ya hapo anaweza kujua aagize oda kiasi gani kupitia kwenye mfumo kwenye simu yake ya kiganjani, ili kumuepusha changamoto.”
Anasema mteja kama anataka kwenda kuchukua mzigo wake, au anakuwa anajua aina ya mzigo anaoenda kuchukua na una ukubwa gani, anaweza kutumia mfumo huo wa MSD Customer Portal .
“Lakini anaweza kuandaa Control number kama anataka kuandaa malipo, endapo akiona akiba yake aliyonayo kwenye akaunti yetu ya MSD haitoshi kuagiza mzigo anaoutaka,” anasema na kuongeza;
“Hivyo anaweza kutemgeneza moja kwa moja control number kupitia mfumo wetu.” Anasema baada ya hapo anaweza kutoa maoni kama amepata huduma sahihi au amekumbana na changamoto gani au kueleza maoni kwa ajili ya kusaidia kuboresha huduma,” anasema Jumaa.
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia