November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kanali Kolombo afungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Kamati za Usimamizi maafa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Pwani

KATIKA kukabiliana na Maafa ndani ya Nchi kuanzia Ngazi za Kitaifa , Mkoa, Wilaya hadi Kitongoji  Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imeendelea kutoa Elimu ya  kukabiliana na Maafa kwa Kamati Elekezi, na Kamati za Wataalamu , Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata katika kujiandaa, kuzuia, kukabili na kurejesha hali pale Maafa yanapotokea.

Akizungumza Julai,Mosi 2024 wakati wa Kufungua Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo juu ya Kupunguza Maafa kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa katika Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Joseph Kolombo amesema mafunzo yamekuja kwa muda muafaka na ni muhimu ambayo yatasaidia kuweza kuchukua hatua za mapema za kuzuia na kupunguza madhara yanapotokea.

“Niwapongeze wote mlioalikwa kuwa sehemu ya mafunzo haya ambayo ni muhimu kwani kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa tutaongeza uelewa na ujuzi kwa shughuli za Usimamizi wa Maafa maana itasaidia kuzuia na kupunguza madhara na itakuwa na gharama nafuu kuliko kusubiri ili kuchukua hatua baada ya maafa kutokea ambapo slSerikali imekuwa ikitumia gharama nyingi kukabiliana na maafa” . Alisema kanali Joseph 

Kwa Upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Luteni Kanali Selestine Masalamado amesema kuwa mafunzo haya ni muhimu ambapo yataweza kuongeza uelewa na ujuzi katika Shughuli za Usimamizi wa Maafa.

“Sote tunakubali kuwa matukio ya Maafa yanatokea na kusababisha madhara katika ngazi ya jamii ambapo Serikali za Mitaa kuanzia kitongoji , Mtaa au Kijiji na Jiji, manispaa zote zinawajibika moja kwa moja lakini sisi tunafurahi kukutana na nyie watendaji katika ngazi hii kwani mnalo jukumu la usimamizi wa maafa katika kujiandaa, kuzuia, kukabili na kurejesha hali,” alisema Luteni Kanali Masalamado

Mafunzo haya ndani ya Wilaya ya kibiti Mkoani Pwani yameanza leo Tarehe 1. Julai 2024 na yanatarajia kumalizika Tarehe 5 Julai 2024.