Na Israel Mwaisaka, Sumbawanga
JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia kijana mmoja mkazi wa Kijiji cha Mtenga Tarafa Namanyere wilayani Nkasi, kwa tuhuma za kumuua kwa kumkata kata mapanga kichwani baba yake mzazi aitwaye Ntemi Seni (65) akidai urithi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo amesema kuwa tukio la kuuawa kwa mzee huyo lilitokea Aprili 25, mwaka huu majira ya saa 09:30 usiku huko Kijiji Mtenga wilayani Nkasi.
Amesema, kijana huyo mwenye umri wa miaka 36 jina linahifadhiwa inadaiwa alikuwa akitaka baba yake mzazi ampe urithi wa mali alizonazo ili ziweze kumsaidia kupata kuendesha maisha yake pasipo utegemezi.
Masejo amesema, baada ya kijana huyo kushinikiza mara kadhaa apewe sehemu ya mali ya mzazi wake kama urithi na baba yake kukataa kufanya hivyo kulizuka vurugu baina yao ndipo kijana huyo alipochukua panga na kuanza kumkimbiza na kisha kumkamata na kuanza kumkata kata na mapanga kichwani.
Kamanda amesema, Baba huyo alivuja damu nyingi katika sehemu ya kichwa na kufariki dunia muda mfupi baadae kutokana na kukosa msaada wa haraka wa kufikishwa hospitalini kwa matibabu.
Amesema, mtuhumiwa huyo anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam