Na David John,TimesMajira,Online Geita
KAMPUNI ya Wachimbaji wa Madini wanawake mkoani Gaita (GEWOMA GOLDMAIN COMPANY LTD) wameiomba Serikali kuwatengea maeneo maalum kwa ajili ya uchimbaji.
Pia wameomba kuwawezesha vifaa vya kuchimbia madini ili kuweza kurahisha upatikanaji wa madini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Geita, Mwenyekiti wa Kampuni, Josepha Lebabu amesema wao kama wanawake waliamua kuazisha kampuni yao kwa lengo la kujikwamua kiuchumi pamoja na kuchangia mapato Serikali ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi kubwa zinazofanywa na Rais John Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele kutaka Watanzania kuondokana na umasikini.
Amesema Rais Magufuli ni kiongozi wa wanyonge na anataka watu wake waweze kujikwamua kiuchumi.
“Hata Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandis Robart Gabriel, amekuwa muhimili mkubwa kwetu kama wanawake wachimba madini mkoani hapa kwani amekuwa akiwapa maelekezo yenye tija na yenye kuleta mafanikio miongoni mwao, hivyo wanampongeza na kumshukuru kwa kazi kubwa anayofanya mkoani Geita,”amesema.
Amesema awali kabla hawajaazisha kampuni walikuwa na ushirika ambapo mwisho wa siku watu walikuwa wanagawanyika hivyo waliona ni vema kuazisha kampuni ambayo ina uwezo wa kuuza hisa na kujumuisha wanawake wote nchini.
“Ndugu zangu waandishi tulifanya maamuzi ya kuazisha kampuni na kuuza hisa kutokana na ushauri wa Serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya madini nchini, Dotto Biteko katika maonesho ya pili yaliyofanyika mwaka jana hapa Geita ambapo baada ya kutembelea banda letu ndipo alishauri tuwe na kitu kama hiki,”amesema Josepa.
Josepha amefafanua kuwa baada ya waziri kutembelea aliwashauri kujiunga pamoja wao kama wanawake wachimba madini na kuazisha kampuni yao ya kuchimba madini, hivyo kwa kufanya hivyo wanaweza kurasimishwa shughuli zao na serikali itawaunga mkono kwa yale ambayo wao wanayafanya.
Amesema baada ya kupokea ya ushauri waliufanyia kazi hivyo wanaiomba Serikali kusaidia maeneo ya wao kuweza kuchimba madini na maeneo hayo yawe tayari yamerasimishwa na watafiti wa madini ili kuepuka hasara ambayo wanaweza kuipata wakati wa kuchimba pasipokujua kama eneo husika lina madini ya kutosha.
“Tunaomba Serikali baada ya kutupa maeneo itusaidie kutukopesha vifaa vya uchimbaji kama vile mashine ya kuvuta maji, mashine ya kucholongea miamba, gari kubwa la kubebea makasha ya kusagia, winchi pamoja na mashine ya kuchenjulia dhahabu,”amesema Josepha.
Wakati huo huo amewataka wanawake kote nchini kununua hisa kupitia kampuni hiyo ya Gewoma Mine Gold Company ltd na kwamba hisa zipo za kutosha, hivyo wanakaribishwa kuchangamkia fursa hiyo.
Amesema wao wanapatikana katika maeneo ya Bomani Center mkoani humo,mtaa wa Kabalila nyumba namba nne kutoka Barabara Kuu ya lami.
Amesema tangu wameazisha kampuni hiyo pamekuwepo na mafanikio makubwa na hata serikalini wameshaaza kulipa mapato hivyo wanawake popote walipo wajitokeze kwa wingi kujiunga nao.
More Stories
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi
Hatma mrithi wa Kinana kupatikana
Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19