Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Chunya
KAMPUNI ya ununuzi wa Tumbaku ya Premium Active Tanzania imetoa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi mil.39 kwa Taasisi za umma katika tarafa ya Kipembawe wilayani Chunya mkoa Mbeya ikiwa ni sehemu ya kampuni hiyo kurejesha faida katika jamii.
Vifaa vilivyotolewa ni Kompyuta, Madawati, Meza, Viti, Saruji, Kabati ya kutunzia taarifa, Mabati, Madirisha, Mashine ya kudurufia mitihani vikilenga kusaidia taasisi za elimu kama vile shule za Msingi, Sekondari pamoja na Ofisi za vijiji katika maeneo yanayolima zao la tumbaku.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya,Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Premium Active Tanzania, Harry Klonaridis amesema kampuni hiyo imekuwa na utamaduni wa kurejesha sehemu ya faida kwenye jamii wanayoshirikiana nayo kwa kipindi kirefu, lengo likiwa kuwasidia wananchi hao kupata maendeleo.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema vifaa vilivyotolewa mwaka huu vinalenga kuboresha sekta ya elimu na kuweka mazingira mazuri kwenye Ofisi za Vijiji ili ziweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi hasa wakulima wa zao la tumbaku.
“Tunaamini msaada huu utawafikia wananchi wengi zaidi hasa wakulima ambao tunafanya nao biashara, lengo letu ni kuona wananchi katika maeneo ambayo kampuni yetu inafanya kazi wanapata maendeleo” amesema Klonaridis
Meneja wa operesheni wa kampuni ya Premium Active Tanzania,Nicco Roussos amesema vifaa hivyo vimenunuliwa kwa kuzingatia mahitaji ya walengwa kama walivyoomba, hivyo anaamini vitasaidia kuleta tija katika sekta ya elimu na uzalishaji wa zao la tumbaku.
Ameivitaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni madawati 75, mashine za kurudufu, kabati, meza na viti vya ofisini yatakayopelekwa katika shule za sekondari na msingi pamoja na meza na viti ambavyo vimeelekezwa kwenye ofisi za vijiji.
Amesema mbali na vifaa hivyo pia wamechonga madirisha ya vyima na aluminium ambayo yatapelekwa katika majengo ya shule na ofisi katika maeneo yenye uhitaji.
Akipokea vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mbarack Alhaj Batenga amesema kitendo cha kampuni hiyo kurejesha sehemu ya faida yake kwa wananchi ni cha kupongezwa na kinachopaswa kuigwa na kampuni nyingine zinazonunua tumbaku wilayani Chunya.
Amesema Kampuni ya Premium Active Tanzania, ni kamupni kongwe ya ununuzi wa tumbaku wilayani Chunya ambayo imeonyesha njia kwa kampuni nyingine ambazo zimesajiliwa kukunua zao hiyo wilayani Chunya.
“Ndani ya Wilaya hii tuna kampuni nne za kununua tumbaku na mwaka huu tumesajili kampuni nyingine mbili, sasa kampuni hii kama kampuni kongwe ya ununuzi wa tumbaku wilayani hapa, wameonyesha njia hivyo na wengine igeni mfano huu kwa manufaa ya wakulima wa zao hili,” amesema Batenga.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, ambaye pia ni Afisa Kilimo wa Wilaya ya Chunya, Cuthbert Mwinuka amewataka wanufaika wa vifaa hivyo kuvitunza na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Amesema kwa kuwa baadhi ya vifaa hivyo ni vya kisasa ikiwa kuna watymiaji ambao hawajui namna ya kuvitumia waende kujifunza ili wavitumie kwa ufasaha badala ya kuviharibu ndani ya uda mfupi.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa vifaa hivyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mayeka, Flora Mwanshuli aliahidi kuvitumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba vitaleta tija hasa katika sekta ya elimu.
More Stories
Waziri Slaa:Anwani za makazi zinarahisisha upokeaji na utoaji huduma
Rais Samia awaonya Majaji na Mahakimu
Mwabukusi akerwa na wanaodai amelamba asali