December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni ya iTrust yazindua mfuko mpya wa uwekezaji wa pamoja

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Kampuni ya iTrust Finance imezindua mfuko mpya wa uwekezaji wa pamoja ambao unakusudia kutoa fursa kwa wawekezaji wengi kuwekeza katika dhamana mbalimbali kama vile hisa, hatifungani, amana za benki, na dhamana nyingine. Mfuko huu unalenga kuwawezesha wawekezaji wadogo na wakubwa kushiriki katika masoko ya fedha na mitaji.

Mfuko huu una sehemu tano tofauti ambazo ni iCash Fund, iGrowth Fund, iIncome Fund, iSave Fund, na iMaan Fund. Kila mfuko una lengo tofauti kulingana na mahitaji ya wawekezaji, kama vile kuimarisha mtaji, kupata mapato au kuweka akiba.

Katika hafla ya uzinduzi wa mfuko huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, CPA Nicodemus Mkama, alieleza kuwa kuanzishwa kwa mifuko hii ni hatua muhimu katika juhudi za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi kote nchini, ikiwa ni pamoja na vijijini, ili kuwasaidia kiuchumi.

Mkama alisema mauzo ya awali ya vipande vya uwekezaji katika mifuko hii yalianza tarehe 12 Novemba 2024, na kampuni inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 37.

Alisema Fedha hizo zitawekezwa katika masoko ya fedha na mitaji, ikijumuisha hisa za kampuni zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa, hatifungani za serikali, hatifungani za kampuni, na dhamana za serikali za muda mfupi.

“Lengo la uwekezaji wa aina hii ni kuifanya mifuko kuwa na ukwasi unaotosha ili kukidhi mahitaji ya fedha za wawekezaji pindi mahitaji yanapotokea. Aidha, kwa upande wa mfuko wa Imaan, fedha zitakazopatikana zitawekezwa kwenye bidhaa za masoko ya mitaji zinazozingatia misingi ya Shariah, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika hatifungani za Sukuk.”

Kadhalika, Mkama alizitaja faida za uwekezaji wa katika mifuko hiyo katika ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi hapa nchini.

“unachangia katika utekelezaji wa Sera ya Serikali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuwezesha makundi mbalimbali ya jamii, ikiwa ni pamoja na watu wa kipato cha chini kuwekeza kwa pamoja katika dhamana za Serikali (Treasury Bonds) ambapo, katika hali ya kawaida wasingeweza kushiriki katika uwekezaji huo, kwani kima cha chini cha ushiriki ni Shilingi Milioni moja. “

“uwekezaji utakaofanywa na Mifuko hii katika hatifungani za Serikali utawezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharamia miradi ya maendeleo kama ambavyo ilivyoainishwa katika Mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo yaani Alternative Project Financing (APF) Strategy.”

“wawekezaji watalipwa gawio kutokana na faida za uwekezaji na wakati huo wakiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na fedha za mifuko kuwekezwa katika hatifungani za Serikali.” Alisema

Mkama alisema Faida nyingine ya kuwekeza katika Mifuko hii ni kuwa vipande vya uwekezaji vinaweza kutumika kama dhamana ili kuwezesha wawekezaji kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Kutokana na hivyo, Mkama aliwataka wadau wote wa masoko ya mitaji kuendelea kushirikiana na CMSA katika kutekeleza mikakati ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, ambayo ndiyo azma na malengo ya Serikali kama ilivyoainishwa katika sera mbalimbali za nchi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Peter Nalitolela alisema uzinduzi wa mifuko hiyo ni njia mojawapo ya taasisi za kifedha kama iTrust kuweza kupanua wigo wake katika uwekezaji katika soko la hisa

“Taasisiz a kifedha zitakapowekeza huwa ni nguvu ya kuanzisha soko, kuongeza ukwasi na kukuza mtaji, Kwahiyo taasisi hizi huwa zinakuwa na nguvu kubwa ya kuweza kuwekeza na hivyo kuweza kufanya ununuaji na uuzaji wa hisa urahisishwe zaidi”

Alisema chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, masoko ya mitaji na dhamana yakiendelea kukua na soko la hisa limekua hadi kufikia juzi jumla ya thamani ya mitaji katika soko la Hisa imefika shilingi Trilioni 18.5

“Mafanikio haya ni jambo jema kwa watanzania kwani wawekezaji ambao wamewekeza katika
Masoko ya mitaji na dhamana wanapata faida hata kwenye uwekezaji wao na thamani ya uwekezaji wao kupanda lakini pia ni faida kwa serikali”

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, ameeleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, uwekezaji nchini Tanzania umepiga hatua kubwa. Teri amesema kwamba mwaka 2020 TIC ilisajili miradi ya uwekezaji yenye thamani ya takribani dola bilioni 2, lakini hadi kufikia Novemba mwaka huu, thamani ya miradi hiyo imefikia karibu dola bilioni 7.

Miradi hii inajumuisha sekta kama viwanda, mashamba makubwa, utalii, uchukuzi, na majengo ya kibiashara, ambayo yamechangia kuongeza ajira na mitaji nchini Tanzania.

Kuhusu uwekezaji wa masoko ya fedha (iTrust), Teri amesisitiza umuhimu wake, akieleza kuwa ili uwekezaji wa kawaida ukue, ni lazima kuwe na fedha za kutosha kwenye uchumi. Uwekezaji huu wa iTrust unaleta fedha muhimu zinazosaidia ukuaji wa uchumi.

Aidha, Mjumbe wa Bodi ya iTrust Finance Limited, Prof. Mohamed Warsame, amewataka Watanzania kuwekeza katika mifuko hiyo mitano ya iTrust kwani inaleta faida kubwa kwa wawekezaji na kuchangia katika maendeleo ya kifedha nchini.