November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni binafsi za ulinzi zaaswa kuzingatia sheria

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Sarige amewata wakurugenzi na wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi kufuata sheria kwa kuwasimamia vyema askari wanaowa ajiri kufanya kazi hiyo.

ACP Sarige ametoa wito Novemba 04, 2023, katika Bwalo la Polisi Mabatini wilayani Nyamagana wakati wa kikao kazi na uongozi wa kampuni hizo pamoja na wamiliki.

Ofisa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhani Sarige

Amewahimiza kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kutoa mafunzo kwa walinzi ili kuleta uelewa wa pamoja na kuimarisha nidhamu kwa askari hao wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Yesaya Suddy akitoa elimu katika kikao hicho amesema katika jamii si ajabu kukutana na mlinzi anayelinda mali yenye thamani ya zaidi milioni mia tano lakini hajui hata kutumia (kukoki) silaha aliyonayo kwenye lindo kitu ambacho ni hatari kwa usalama.

Naye, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ilemela Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Ignatus Kapila amewataka wamiliki kutoa elimu kwa walinzi kwa kushirikiana katika lindo kwani sio jambo jema kuona lindo la jirani linavamiwa bila kutoa msaada na kuishia kuangalia tu.

Hata hivyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana Mrakibu Msaidizi wa Polisi, (SP), Virginia Sodoka amesema wataanza kuchukua hatua kali za kisheria kwa wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi watakaoendelea kukiuka sheria na taratibu za nchi.

Mkuu wa Upelelezi makosa ya jinai Mkoa wa Mwanza Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Yesaya Suddy

Kwa upande wao viongozi wa kampuni binafsi za ulinzi wameahidi kwenda kutekeleza yale yote yaliyoadhimiwa katika kikao hicho ili kuboresha utendaji wa askari wa kampuni hizo ikiwa ni pamoja na kuangalia masilahi yao.

Mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi binafsi, Bandit Security Company Limited, Salum Mparo, amesema wanaendelea kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Ulinzi Rasilimali Watu Kanda ya Ziwa (TAMASCA), Charles Chacha amesema elimu waliopata ni nzuri na itawasaidia wakurugenzi wa kampuni za ulinzi binafsi kutenda kazi zao za kila siku kwa kuwakumbusha wajibu wa utendaji kazi walinzi wao wanapokuwa lindoni.