March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni ya Yas ‘Anzia Ulipo’ yatua mkoani Morogoro

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya mawasiliano inayoongoza nchini, Yas, imeendeleza Kampeni yake ya nchi nzima inayofahamika kama ‘Anzia Ulipo’, kwa wakazi wa Morogoro.

Hiyo ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuwawezesha Watanzania – hasa vijana na wajasiriamali – kutimiza ndoto zao kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Yas, Isack Nchunda, amesema kampeni hiyo ni mwendelezo wa dhamira ya Yas kuwa mshirika wa kweli wa Watanzania katika safari ya mageuzi ya kidijitali.

“Anzia Ulipo ni wito wa matumaini kwa kila Mtanzania mwenye ndoto. Tunaamini kwamba mafanikio yanaanzia pale ulipo kwa kile ulicho nacho na Yas ipo bega kwa bega kuhakikisha unafikia malengo yako,” amesema Nchunda.

Kwa mujibu wa Nchunda, kampeni hiyo inalenga kuwawezesha vijana kutumia miundombinu ya kisasa ya kidijitali ya Yas, ambayo kwa sasa imeenea kila kona ya nchi kupitia mitandao ya kasi ya 4G na 5G, ili kuendesha shughuli za biashara, kupata maarifa, na kushiriki katika uchumi wa kisasa.

“Miundombinu yetu ya mawasiliano ni uti wa mgongo wa sekta muhimu kama afya, elimu, kilimo na biashara. Leo hii, kijana wa hapa Morogoro anaweza kuuza bidhaa zake nje ya nchi kwa kutumia simu ya mkononi,” ameongeza.

Yas pia, imetambua nguvu ya vijana katika maendeleo ya taifa, ikizingatia kuwa zaidi ya asilimia 34 ya Watanzania wako kati ya umri wa miaka 15 hadi 35.

Katika kundi hilo, wengi wamekumbatia ujasiriamali wa kidijitali – kuanzia teknolojia ya kilimo (agritech), ubunifu wa mitindo, hadi uundaji wa maudhui mtandaoni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Pwani-Kaskazini, Abdul Ally, amesisitiza kuwa uzinduzi huu unaakisi dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kushirikiana kwa karibu na jamii kwa kutoa huduma bora zinazowagusa watu moja kwa moja.

“Kama kampuni, tunatambua umuhimu wa kuwa karibu na wateja wetu. Uzinduzi huu sio tu wa kampeni, bali ni uthibitisho wa kwamba Yas iko tayari kuwahudumia Watanzania kwa ukaribu zaidi – kwa bidhaa, huduma na hata mawazo mapya ya kuboresha maisha ya kila siku,” amesema Ally.

Aidha, ameeleza kuwa kwa mikoa ya ukanda wa Pwani-Kaskazini, ikiwemo Morogoro, kampuni imewekeza katika miundombinu ya mawasiliano na vituo vya huduma kwa wateja ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kunufaika na mapinduzi ya kidijitali.

“Tunawakaribisha wananchi wote wa Morogoro na mikoa ya jirani kujiunga na Yas. Kampeni hii ni fursa ya kila mmoja kuchukua hatua sasa – kuanzia alipo – kuelekea mafanikio ya kidijitali,” ameongeza.

Kampeni ya Anzia Ulipo inatarajiwa kuzunguka mikoa mbalimbali nchini, ikihamasisha Watanzania kutumia fursa za kidijitali kujikwamua kiuchumi, kijamii na kielimu.