Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
BENKI ya Exim Tanzania, kwa kushirikiana na Mastercard, wamezindua rasmi Kampeni ya UEFA Priceless, mpango kabambe unaolenga kuhamasisha matumizi ya Exim Mastercard huku ukiwapa wateja fursa ya kushinda zawadi ya kipekee. Kampeni hii, itakayodumu hadi Aprili 30, 2025, itawazawadia watumiaji wa Mastercard safari ya kifahari iliyolipiwa kikamilifu kwenda Amboseli, Kenya kwa ajili ya kushuhudia mechi ya fainali za UEFA kupitia usiku wa kipekee wa ‘UEFA Finals Screening Experience’.

Akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari, Silas Matoi, Mkuu wa Idara ya Njia Mbadala za Kidijitali wa Benki ya Exim, alisisitiza dhamira ya benki hiyo ya kuhamasisha matumizi salama na rahisi ya miamala ya kidijitali. “Ushirikiano huu na Mastercard unathibitisha dhamira yetu ya kuwapatia wetu suluhisho bora za kifedha kwa njia ya kidijitali. Kwa kuhamasisha matumizi ya kadi, tunawawezesha wateja wetu kufurahia huduma zenye urahisi zaidi huku tukichangia ukuaji wa uchumi usiotegemea fedha taslimu nchini Tanzania.”
“Mshindi wa kampeni hii atapata safari ya kifahari ya siku tatu na usiku mbili kwenda Amboseli, Kenya kuanzia Mei 30 hadi Juni 1, 2025, akiwa na watu wake wa karibu watatu. Zawadi hii inajumuisha malazi ya kifahari katika hoteli ya Serena Amboseli, usafiri wa binafsi kutoka Nairobi hadi Amboseli, safari ya kipekee ya kutalii, na safari maalum ya angani kwa kutumia puto ya Mastercard. Tumekamilisha taratibu zote ili kuhakikisha kampeni hii inakidhi vigezo vya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania,” aliongeza Silas.
Naye Meneja wa Akaunti ya Mastercard Tanzania, Moses Alphonce James, alielezea furaha ya kampuni hiyo kushirikiana na Benki ya Exim kuwaletea Watanzania fursa hii adhimu. “Mastercard imejikita katika kuunda uzoefu wa thamani kwa wateja wetu. Kwa kuunganisha matumizi ya kadi na tukio la kipekee la UEFA, tunafanya miamala ya kila siku kuwa na maana zaidi huku tukihamasisha matumizi bora ya kifedha kwa njia salama na za kisasa.”

Zaidi ya zawadi zinazotolewa, kampeni hii pia inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Mastercard, taasisi za kifedha, wafanyabiashara, na wateja. Kwa kuhimiza njia salama za malipo, mpango huu utawezesha Mastercard kuboresha huduma zake za baadaye na kuimarisha suluhisho za kifedha za kidijitali katika sekta ya fedha inayokua kwa kasi nchini Tanzania.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano, Kauthar D’souza kutoka Benki ya Exim, alisisitiza jinsi kampeni hii inavyoleta athari chanya kwa wateja wa benki hiyo. “Sisi kama Benki ya Exim, tunajitahidi kila mara kuwapatia wateja wetu fursa za kipekee zaidi ya huduma za kibenki za kawaida. Kampeni hii inawawezesha wamiliki wa kadi zetu kufurahia manufaa maalum wanapofanya miamala yao ya kila siku. Tunawahimiza wateja wetu wote kushiriki na kupata nafasi ya kushinda safari hii ya kipekee isiyosahaulika.” Benki ya Exim inaendelea kupanua huduma zake za kifedha kwa njia ya kidijitali, na ushirikiano huu na Mastercard unadhihirisha dhamira yake ya kutoa suluhisho bunifu za kifedha zinazoboresha maisha ya wateja wake. Watumiaji wa Mastercard za Benki ya Exim wanahimizwa kufanya miamala zaidi kwa kutumia kadi zao kabla ya Aprili 30, 2025, ili kupata nafasi ya kushinda safari hii ya kipekee.
More Stories
Kamati ya kudumu ya Bunge yapongeza ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati Mtumba
Gawio kutoka kampuni ambazo Serikali ina hisa chache zapaa kwa asilimia 236
Pinda:Vijana tumieni fursa kupata maarifa ya ufundi stadi