Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline
KAMPENI ya Mama Samia Legal Aid (MSLAC) ilivyoanzishwa mapema mwaka jana na Wizara ya Katiba na Sheria imeleta manufaa makubwa muda mfupi tangu kuanzishwa kwake kwa watu wengi kunufaika na msaada wa kisheria unaotolewa bure.
Tangu ilipozinduliwa Aprili mwaka jana jijini Dodoma imeshawanufaisha wananchi zaidi ya 494,000 kutoka katika mikoa saba, wamepata suluhisho la migogoro huku migogoro ya ardhi ndio ikiongoza.
Kampeni hiyo imeshafikia mikoa saba, halmashauri 42, kata 452, na vijiji/mitaa 1,348 ambayo imewagusa wananchi kwa kuwapa msaada wa kisheria bure miongoni mwao wakiwemo wafungwa na mahabusu.
Takwimu za MSLAC zinaonesha kuwa wafungwa 7,166 wanaume wakiwa 6,824 na wanawake 342 walifikiwa na kupewa msaada wa kisheria kwenye magereza mbalimbali nchini.
Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi alitoa maelezo haya mwishoni mwa wiki wakati akizungumza kwenye banda la Mama Samia Legal Aid Campain katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaama(DITF) yanayoendelea barabara ya Kilwa wilayani Temeke.
Anasema ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi kwa urahisi zaidi mashirika 256 yamesajiliwa kwaajili ya kutoa msaada kwa wananchi bila kuwatoza gharama kwani serikali imeamua kuwasaidia.
Ester ambaye pia ni Msajili wa Mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria, alisema baadhi ya migogoro ambayo imetatuliwa kupitia kampeni hiyo ni ile inayohusu ushauri wa msaada wa kisheria, kuelimishwa kwa suala lolote la kisheria pale wanapohitaji kuwasilisha mahakamani, kuwaunganisha na Mawakili, kuandaliwa nyaraka na huduma nyinginezo zinazohitaji kutatuliwa kisheria.
“Kwa hiyo Wizara iliona umuhimu wa kuleta kampeni hii ya kitaifa ya msaada wa kisheria ambayo imepewa jina mama Samia legal Aid Campain katika maonesho haya ya sabasaba kutokana na umuhimu wake katika kutatua migogoro ya wananchi na kampeni hii inatolewa bure,”alisema Eater.
“Kwa hiyo tuko hapa kuungana na wadau wengine katika kuhakikisha mwananchi hakosi huduma yoyote ya kisheria akiwa katika viwanja hivi vya sabasaba, kwa hiyo kama kuna mtu ana jambo lake linamtatiza na anataka litatuliwe kisheria atumie fursa hii ya maonesho,tuko mpaka mwisho kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi zaidi.”
Alisema kesi ambazo wakili anaweza kumsaidia mwananchi baada ya kufika katika kampeni hiyo ya kitaifa ni pamoja na hati za kufungua mashauri mahakamani iwe ni kufungua kuomba usimamizi wa mirathi, masuala ya madai,matunzo ya watoto, kuasili watoto na masuala mengine ya kisheria ambayo nyaraka zake zinapelekwa mahakamani.
Anasema pia ipo mikataba ambayo mtu anaweza kusaidiwa kuandika pamoja na huduma nyingine ambazo mwananchi wa kawaida hawezi kwenda kuzipata kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumlipa wakili.
Ester anasema tangu yalipoanza maonesho ya sabasaba Juni 28 mwaka huu, mwitikio wa wananachi wanaojitokeza kuomba kutatuliwa migogoro yao inayohitaji msaada wa sheria ni mkubwa.
“Wananchi waliojitokeza ni wengi tangu tumefika hapa Juni 28 na hii inatuonesha kwamba huduma zetu zimefika mbali sana na wananchi wamepata taarifa kwa hiyo kadiri muda unavyoenda na idadi ya wananchi wanaokuja hapa inaongezeka,”alisema Ester.
Anasema wananchi wanapopata elimu ya kisheria na ushauri, wanakuwa na uwezo wa kuelewa taratibu za kisheria na haki zao, hivyo kupunguza malalamiko na migogoro isiyokuwa na ulazima.
“Kampeni hii inalenga kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi kwa njia rahisi na ya karibu. Kupitia kliniki za ushauri na elimu ya sheria, wananchi watapata fursa ya kushauriwa na wataalamu wa sheria bila malipo,” anasema
Anasema kampeni hiyo inalenga pia kujenga jamii yenye ufahamu zaidi na yenye uwezo wa kudai na kulinda haki zao za ardhi kwa mujibu wa sheria Kukuza usawa na haki katika jamii, kuheshimu matakwa ya marehemu, kuzuia migogoro ya mirathi, na kusimamia mali kwa njia inayofuata sheria na haki za kila mmoja.
“Wananchi wanahitaji msaada wa kisheria ili kupata haki zao kwa hiyo hii kampeni inatoa msaada wa kisheria kupitia vituo vya msaada, mawakili, na elimu ya kisheria, ikilenga migogoro ya ardhi, urithi, na haki za binadamu na inaongeza uelewa wa sheria na upatikanaji wa haki nchini Tanzania,” anasema.
Mama Samia Legal Aid Campain ilianza kutekelezwa Aprili mwaka jana kwa kuanzia mkoani wa Dodoma na mpaka sasa tayari mikoa saba imefikiwa.
Mbali na Dodoma mikoa mingine iliyofikiwa ni, Manyara, Singida, Simiyu, Shinyanga na Njombe na Ruvuma.
Kampeni hiyo inachangia utawala bora ambao unajumuisha uwazi, uwajibikaji, na ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi na utekelezaji wa sheria na sera za umma.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia