Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Morogoro
WIZARA ya Katiba na Sheria inatarajia kufanya operesheni maalum wilayani Kilosa mkoani Morogoro ya kutatua migogoro papo kwa papo,kwa kishirikisha wataalam wa sekta mbalimbali ikiwemo mahakama inayotembea.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Damas Ndumbaro,amesema hayo Kata ya Magomeni wilayani Kilosa mkoani Morogoro,wakati  akizindua kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia Legal Aid wilayani humo na kuahidi kuongoza oparesheni hiyo.
Amesema operesheni hiyo itakayoanza baada ya siku kumi za kampeni ya msaada wa Kisheria kwa Mkoa wa Morogoro,zinapanga kutatua changamoto zinazoikabili Wilaya ya Kilosa ambayo imeshika kasi katika migogoro ya ardhi na ile ya wakulima na wafugaji.
Ameitaka ofisi ya  Mkuu wa Wilaya ya Kilosa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuwa tayari kwa zoezi hilo, ikiwemo kuwaandaa walalamikaji, walalamikiwa na mashahidi katika maeneo yenye migogoro ili wasikilize na kuamua papo hapo na ambaye hataridhika na maamuzi aweze kusogea penye mahakama inayotembea.
“Nimepokea maombi na ushaurii  ulliotolewa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Kilosa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Prof.Paramagamba Kabudi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa,Shaka Hamdu Shaka na tufanaya oparesheni hii zikimaliza siku 10 za kampeni, na mimi ndiye nitaongoza,”amesisitiza.
Amesema maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha elimu ya msaada wa kisheria inawafikia wananchi wengi hasa wasio na uwezo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili bila gharama.
Pia amesema,migogoro mingi kwenye jamii inachangiwa na watu kutojua haki na wajibu wao pamoja na sheria, lakini kupitia elimu ya msaada wa kisheria wengi watajua hatua za kufanya na kuondoa au kupunguza migogoro iliyopo kwani inachangia uvunjifu wa amani na kukosesha maendeleo ya watu wa maeneo husika.
Naye Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Mochezo Prof.Paramagamba Kabudi,amesema  tayari Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Waziri wake Dkt.Ashatu Kijaji imetangza Wilaya ya Kilosa kuwa Kanda maalum ya kushughulikia matatizo ya wakulima na wafugaji,kutokana na Wilaya hiyo kuongoza kwa migogoro ya ardhi na ya wakulima na wafugaji.
Aidha amesema Mawaziri mbalimbali wamekusudia kwenda wilayani Kilosa ili kushughulikia changamoto zilizopo akiwemo Waziri wa Kilimo, Waziri wa Ardhi na Waziri wa Mifugo .
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima,amesema simu nyingi anazopokea za malalamiko Wilaya inayoongoza ni Kilosa ikifuatiwa na Kilombero.
“Wakati mwingine migogoro mingi ni kutokana watu kukosa elimu ya sheria na kushindwa kujua tatizo lake linapaswa kutatuliwa na mamlaka zipi,kwani mengine ni masuala ya kisheria,”amesema Malima na kukiri kuwa Wilaya ya Kilosa ni kubwa ikiwa na kilometa za mraba12,000 na wanahitaji zaidi huduma hizo za msaada wa kisheria kwa upana wake.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka,amesema licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali kwa wananchi wa Kilosa ikiwemo miradi katika sekta mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya bilioni 63,lakini migogoro ya ardhi na ya wakulima na wafugaji bado imeshika kasi wilayani humo.
 Hata hivyo akasema uwezo mdogo wa wananchi,kumefanya wengi kushindwa kupata haki stahili na kwamba asilimia zaidi ya 85 ya migogoro watakayopokea  wataalam katika kampeni hiyo itahusu ardhi na ya wakulima na wafugaji.
“Wilaya ya Kilosa ni kubwa,ili wananchi wengi zaidi wa vijijini wenye uhitaji wafikiwe, tunaomba tuongezewe mudavijiji na Kata zaidi katika kampeni hii,”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Shaka pia akaiomba  wizara ya Katiba kuongeza wanasheria zaidi katika ofisi ya Mashtaka wilayani humo kwani  kesi zilizopo ni nyingi na zinahitaji utatuzi,ambapo kwa sasa kuna kesi karibu 260 zilikuwa bado kwenye utaratibu wa kwenda mahakamani.
More Stories
Handeni waridhishwa na World Vision utekelezaji wa miradi
Prof.Muhongo atunukiwa tuzo ya pongezi Musoma Vijijini
PPAA yaokoa bilioni 583