January 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni ya Mama Samia kutikisa mikoa sita

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline

KAMPENI ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inatarajiwa kuzinduliwa tarehe 24 mwezi huu katika Mikoa sita ambayo itaanzia mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Mtwara.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Alisema katika utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria Wizara imepanga kuifikia mikoa sita ambayo ni Kigoma, Kilimanjaro, Geita, Katavi, Tabora na Mtwara na kuzifikia Kata 10 kwa kila Halmashauri za Mikoa tajwa.

Alisema timu za wataalamu katika sekta ya Sheria itaweka kambi kwa muda wa siku 9 katika Mikoa hiyo na Huduma za Msaada wa Kisheria zitatolewa bila malipo.

Alisema tarehe 25 Januari kampeni hiyo itazinduliwa katika Mkoa wa Geita, na baadaye tarehe 29 zitazinduliwa katika Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba uzinduzi huo utafuatiwa na utolewaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa siku 9 katika maeneo hayo na kuzifikia Halmashauri zote za Mikoa sita.

“Nitoe rai kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kupata huduma za msaada wa kisheria wakati wote wa Kampeni. Katika kipindi cha utekelezaji wa Kampeni, timu ya wataalam zitakuwa uwandani katika Halmashauri zenu na niwaombe mfuatilie matangazo ya vyombo vya habari na Uongozi wa Mitaa ili kufahamu sehemu ambazo watoa Huduma watakapokuwa,”alisema Dk. Ndumbaro.

Aidha, alisema sambamba na utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria, Wizara kupitia Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki itakuwa inafanya mafunzo kwa Kamati za usalama katika ngazi ya Mikoa na Wilaya na pia kuwajengea uwezo wataalamu wa halmashauri na watendaji wa Kata kuhusu elimu ya urai na utawala bora lengo ikiwa ni kuwawezesha katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi kwa ufanisi na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu,” alisema.

“Ninapomaliza taarifa hii, Ninawashukuru sana kwa kuendelea kushirikiana na Wizara katika kutoa habari za shughuli zinazofanywa na Wizara ikiwemo utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Niwaombe mara baada ya kumaliza mkutano huu tufikishe habari hizi kwa wananchi ili waweze kuitumia Kampeni ya Msaada wa Kisheria katika kusuluhisha migogoro inayojitokeza na kupata suluhu,” alisema.

Alisema Wizara ya Katiba na Sheria katika kuweka mwendelezo wa utatuzi wa migogoro hata baada ya kumalizika kwa Kampeni Wizara imeanzisha Madawati ya Msaada wa Kisheria yanayopatikana katika Halmashauri zote Nchini ambayo yanatoa Msaada wa Kisheria bila Malipo,” alisema.

Aidha, Dkt. Ndumbaro alisema yapo mashirika yanayotoa msaada wa Kisheria yenye mawakili, wanasheria na wasaidizi wa kisheria nchi nzima ambayo nayo majukumu yao ni kuhakikisha wananchi wanasikilizwa na kupatiwa huduma za msaada wa Kisheria ili haki itendeke kwa kila Mwananchi mwenye uhitaji,” alisema.