November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamishina Luoga awataka wataalam Wizara ya Nishati kuwafikishia wananchi huduma

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMISHNA wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amewataka Wataalam wa Wizara ya Nishati na taasisi zake kujikita katika kufanya kazi kwa kasi, umakini na bidii ili kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika.

Ili kitenfo hicho kiwe kipimo kikuu
cha kutangaza kazi za Wizara kwa wananchi.

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (kulia)akipata maelezo kuhusu nishati safi ya kupikia katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam. Anayetoa maelezo ni Adelina Lyakurwa, Ofisa Masoko Mwandamizi kutoka TANESCO.

Kamishna Luoga ameyasema hayo alipotembea Banda la Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar-es-Salaam.

“Wizara ya Nishati tumejipa changamoto ya kuongeza bidii zaidi ya
kufanya kazi na kutoa huduma bora kwani Watanzania wanachotaka ni nishati ya kutosha ikiwemo ya umeme bila kuwa na usumbufu wowote,”amesema Mha.Luoga

Ameeleza kuwa, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa inatoa fedha za kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji umeme pamoja na miradi mingine ya nishati akitolea mfano mradi wa umeme wa Julius Nyerere
(JNHPP), unaotekelezwa kwa kiasi cha trilioni 6.5 ambao sasa umefikia asilimia 98.

Ametaja baadhi ya miradi mingine ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa
kuwa ni pamoja na ya usafirishaji umeme itakayounganisha Mkoa wa Katavi na Kigoma kwenye gridi ya Taifa.

Ambapo mradi huo ni kutoka Tabora hadi Katavi na Tabora hadi Kigoma pamoja na miradi ya kuboresha upatikanaji umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Ameeleza kuwa, maonesho hayo ni muhimu kwani Serikali inapata wasaa wa
kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu yake kwa wananchi na kupata mrejesho wa huduma inazotoa, suala ambalo ni muhimu katika kupima utendaji kazi.

Kuhusu utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, Mha. Luoga amewaasa wananchi kutumia nishati ilio safi huku akiwahamasisha kutumia majiko ya umeme yanayouzwa kwa gharama nafuu, yanatumia umeme kidogo na kupika chakula kwa muda mfupi ikiwa ni matokeo ya teknolojia mpya iliyobuniwa na TANESCO kwa kushirikiana na kampuni ya TaTEDO na SESCOM.

“Nimetembelea mabanda ya Maonesho ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake na kuona jinsi Wataalam wanavyohudumia wananchi kwa umahiri na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo za kuunganisha umeme, kuonesha wananchi kwa vitendo matumizi ya nishati safi ya kupikia na kutatua changamoto mbalimbali ambazo wananchi wanaziwasilisha,”ameeleza.

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (kulia)akipata maelezo kuhusu masuala ya usalama wakati alipotembelea banda la Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar-es-Salaam. Anayetoa maelezo ni Ofisa Mwandamizi Afya na Usalama mahali pa kazi kutoka TANESCO, Nelson Boniface

Aidha, amewataka wadau wa nishati hiyo kuhakikisha wanakuwa na kanzidata itakayo jumuisha masuala mbalimbali ikiwemo idadi ya wananchi wanaotumia nishati ilio safi, matumizi yake na kadhalika ambayo itatumika kama moja ya njia za kujitathmini katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha mkakati huo kutekelezwa kwa ufanisi.