Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya
UWAZI wa bei ya dhahabu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya umeongeza uadilifu katika biashara ya madini na kupunguza kwa kiasi kikubwa utoroshaji wa dhahabu nje ya wilaya.
Hatua hiyo imechangiwa zaidi na uwepo wa soko rasmi la madini pamoja na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya shughuli zao Chunya.
Akizungumza Novemba 20, 2025 kuhusu mwenendo wa ukusanyaji wa mapato, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamim Kambona amesema sekta ya madini hasa dhahabu inaendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya halmashauri hiyo, sambamba na sekta ya kilimo.
Kambona amesema kuwa uwepo wa migodi miwili mikubwa ya Kopa na Ujenzi umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato katika halmashauri, huku takribani asilimia 30 ya mapato yote yakitokana na dhahabu.
“Kwa sasa bei ya dhahabu imeimarika na kufikia takribani shilingi 300,000 kwa gramu moja. Hili limetokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya madini. Uwazi wa bei umeondoa mianya ya udanganyifu na kupunguza utoroshaji wa dhahabu,” amesema Kambona.
Aidha, amesema kuwa soko la dhahabu limekuwa likivutia wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali, jambo ambalo limeongeza hamasa ya wachimbaji na wauzaji kufanya biashara ndani ya soko hilo badala ya kutorosha madini.
Hata hivyo, Kambona amekiri kuwa idadi kubwa ya wafanyabiashara imeanza kuelemewa na uwezo wa soko hilo, hivyo halmashauri imepanga kuongeza ghorofa moja ili kupanua nafasi na kuboresha mazingira ya biashara.
“Mapato ya Halmashauri ya Chunya yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka ,mwezi hadi mwezi. Ndiyo maana kwa upande wa madini, Chunya inajulikana kama ‘Mkoa wa Dhahabu,” ameongeza .
Kwa upande mwingine, Hamis Juma mkazi na mfanyabiashara wa nguo Chunya, amesema uchumi wa maeneo hayo umeimarika kutokana na mzunguko mkubwa wa fedha unaotokana na shughuli za madini.
“Uwepo wa madini ya dhahabu ni fursa kubwa Vijana na wanawake wengi wamepiga hatua kimaisha hata uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hii upo vizuri katika kujipanga .
Mzunguko wa fedha ni mkubwa sana na hata sisi wafanyabiashara wa nguo tunafaidika kwa kuongezeka kwa wateja kutoka ndani na nje ya wilaya,” amesema.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina