January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati za ulinzi kwa wanawake na watoto ni njia ya kutokomeza ukatili

Na Penina Malundo,timesmajira,online
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Abeda Rashida amesema uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi kwa wanawake na watoto ni njia mojawapo ya kusaidia kwa kiasi kikubwa kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto nchini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kitaifa kuhusu ajenda ya Mwanamke,Amani na Usalama nchini, Rashida amesema hadi sasa kuna takribani kamati za ulinzi 18,186 kuanzia ngazi ya kijiji  na mtaa hadi ngazi ya taifa zinahitajika kamati 20,750.
Amesema kamati hizo zinamchango  mkubwa katika kuleta amani na usalama kwa wanawake na watoto.”Katika jamii yoyote ile amani na usalama ni suala muhimu kwa ustawi na maendeleo ya jamii,kwani suala la amani na usalama ni matokeo ya ushiriki na ushirikishaji wa wanawake na wanaume katika majadiliano ya amani,ujenzi wa amani na udhibiti wa viashiria vya migogoro katikla jamii na taifa kwa ujumla,”amesema.
Aidha amesema Serikali itaendelea kuratibu na kuandaa mpango kazi wa kitaifa wa amani na usalama kwa wanawake nchini  ambapo jukumu hilo ni shirikisho na jumuishi na serikali italitekeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo shirika la UN Women,Taasisi ya Mwalimu Nyerere,Wizara za kisekta za Kiraia na Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
”Kuandaa mpango kazi wa kitaifa wa amani na usalama kwa wanawake ni hatua muhimu ya jitihada za nchi katika kutekeleza nguzo nne za Azimio Na.1325 la baraza la usalama la umoja wa mataifa kuhusu uzingatiaji wa amani na usalama kwa wanawake,”amesisitiza
Amesema ushiriki wa wanawake katika utatuzi wa migogoro na michakato ya amani,uzingatiaji wa jinsia katika mipango ya kuzuia migogoro,ulinzi wa haki na staha ya miili ya wanawake katika mazingira ya amani na vita,upatikanaji wa huduma nafuu kwa wahanga wa ukatili wa kingono na ukatili wa jinsia ni njia sahihi katika kuendeleza amani na usalama katika kulindsa kundi la wanawake.
”Tunashukuru nchi yetu haina vita ni muhimu kuendelea kulinda amani na kuepusha migogoro kuanzia ngazi ya familia na jamii,”amesema
Kwa Upande wake Mwenyekiti mwenza wa Mtandao wa Sisters Without Borders nchini upande wa Zanzibar,Hashim Pondeza amesema mkutano huo unashirikisha wadau mbalimbali kutoka kwenye mashirika yasiyo ya Kiserikali ,Wawakilishi kutoka Wizara za kisekta ,Mashirika ya Kimataifa ,Taasisi za Umma,Mamlaka za Serikali za Mitaa,wanufaika wa Mradi wa mwanamke na amani pamoja na  balozi mbalimbli.
Amesema wadau hao watashirikiana katika mdahalo mdogo wa kujadili ni namna gani wanakuwa na mikakati ya pamoja katika kuhakikisha uimarishaji wa suala la amani na usalama kwa wanawake linazingatiwa.