December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya ufundi ya Serikali Mtandao itakavyoimarisha jitihada za Serikali Mtandao

Na Mwandishi Wetu,e-GA

Kamati ya ufundi ya serikali mtandao imefanya kikao cha kwanza na kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ya utekelezaji wa majukumu yake, ili kuhakikisha jitihada za serikali mtandao zinaimarika na kuleta tija kwa Umma.

Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) jijini Dodoma, na kuongozwa na Kaimu Mwenyekiti Eric Kitali ambaye ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Eric amesema kamati hiyo ipo kwa mujibu wa kifungu Na. 17 cha sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019, ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kutoa ushauri wa kitaalamu, ili kuhakikisha utekelezaji wa Serikali Mtandao unakuwa ni wenye tija na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.

Amesema kuwa, kamati hiyo ina wajumbe wachache ikilinganishwa na idadi ya Wizara na Taasisi za serikali zilizopo, na kuwasihi wajumbe wote kutenda haki kwa kuwajibika na kuhakikisha wanatoa ushauri wenye tija katika eneo la TEHAMA ili kuhakikisha serikali mtandao inaimarika na kuleta tija kwa Serikali.

“Ikiwa kamati hii itafanikiwa kuifanya mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma izungumze tutakuwa tumeisaidia sana serikali, kwani itaokoa rasilimali fedha pamoja na rasilimali watu”, amesisitiza

Akiyataja baadhi ya majukumu ya kamati hiyo kwa mujibu wa kifungu Na 17 (4) cha Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019, Katibu wa Kamati hiyo Sylvani Shayo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Usalama wa TEHAMA e-GA alisema ni pamoja na; kupitia na kutoa mapendekezo juu ya Sera ya Serikali Mtandao itakayotekelezwa katika taasisi za umma, kupitia na kutoa mapendekezo juu mpango mkuu wa Serikali mtandao na mkakati wake utakaotekelezwa na taasisi zote za umma, kupitia na kutoa mapendekezo juu ya miradi na program za kitaifa za serikali mtandao, na kutoa miongozo ya kiufundi katika kutatua migogoro kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya TEHAMA katika taasisi za umma.

Majukumu mengine ni kuishauri kamati ya kitaifa ya serikali mtandao kuhusu masuala ya serikali mtandao, kuandaa ripoti za robo mwaka na kuziwasilisha katika kamati hiyo, pamoja na kutekeleza majukumu mbalimbali yatakayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao na kamati ya kitaifa ya Serikali Mtandao.

Aidha, kamati hiyo imeazimia kuweka mikakati ya kupunguza urudufu wa mifumo na kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA, katika taasisi za umma inawasiliana na kubadilishana taarifa kupitia Mfumo Mkuu wa ubadilishanaji taarifa serikalini (GoVESB).

Katika hatua nyingine, kamati imemchagua Connie Francis Mkurugenzi wa TEHAMA Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Wajumbe wa kamati hiyo ni Wakuu wa TEHAMA kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali wakiongozwa na Mwenyekiti Bw. Priscus Kiwango kutoka Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Katibu Bw. Sylvani Shayo ambaye ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Usalama wa TEHAMA Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).

Wajumbe wengine ni kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Uratibu na Bunge, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya, Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,

Wizara ya Maji, Mamlaka ya Serikali Mtandao , Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), The Nelson Mandela African Institution of Science and Technology (NM-AIST), Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Ufilisi na udhamini (RITA), Idara ya Uhamiaji, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na Wizara ya Kilimo.