Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) leo itaanza rasmi kusikiliza mapingamizi yaliyowekwa na wadau mbalimbali kwa wagombea kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo ulioangwa kufanyika Agosti 7 jijini Tanga.
Jana saa 10:00 jioni Kamati hiyo ilifunga rasmi mchakato wa kupokea mapingamizi mbalimbali zoezi ambalo limedumu kwa siku tatu kuanzia Juni 19.
Mapingamizi hayo yatawahusu wagombea 20 wa nafasi ya urais pamoja na wanaowania nafasi katika Kamati Tendaji ambao walipita kwenye mchujo wa awali huku pia ikitarajiwa baadhi na mapingamizi kutolewa na wale 12 walioenguliwa katika mchujo wa awali kama yatakuwepo.
Hadi sasa waliobaki katika kinyang’anyiro cha urais ni Hawa Mniga, Evance Mgeusa na Wallace Karia huku kwa upande wa Kanda namba moja ni Athumani Kambi, Lameck Nyambaya na Hosseah Lugano huku kwa upande wa Kanda namba mbili waliokidhi vigezo ni Khalid Mohamed na Zakayo Mjema.
Kwa Kanda namba tatu waliopita ni Abousufian Sillia, James Mhagama na Mohamed Mashango, kwa Kanda namba nne ni Hamisi Kitila, Mohamed Aden na Osuri Kosuri wakati kwa upande wa Kanda namba tano inayoundwa na Mikoa ya Geita, Kagera, Mara na Mwanza waliopita ni Salum Chama, Vedastus Lufano na Salum Kulunge na kwa kanda namba sita yenye Katavi, Kigoma, Rukwa na Tabora waliopita ni Blassy Kiondo, Issa Bukuku na Kenneth Pesambili.
Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, usaili wa wagombea waliovuka kwenye mchujo wa awali utafanyika Juni 25 hadi 27 na matokeo ya awali ya usaili huo yatabandikwa Juni 28 na Juni 30 hadi Julai 2, Sekretarieti watawasilisha masuala ya kimaadili kwenye Kamati ya maadili.
Julai 3 hadi 7 kitakuwa ni kipindi cha kupokea, kusikiliza na kutolea uamuzi masuala ya maadili na kisha Kamati ya maadili ya TFF itatangaza matokeo ya uamuzi Julai 10 na Julai 11 hadi 13 kitakuwa ni kipindi cha kukata rufaa kwa uamuzi wa masuala ya kimaadili kwenye kamati ya Rufani ya TFF.
Julai 14 hadi 18 kitakuwa ni kipindi cha kusikiliza rufani ambapo kipindi cha kukata rufani dhidi ya kamati ya uchaguzi kitaanza Julai 22 hadi 24 na zitasikilizwa kati ya julai 24 na 28.
Wagombea na Kamati ya uchaguzi watajulishwa uamuzi wa Kamati Julai 29 na 30 orodha ya mwisho ya wagombea itatolewa na kisha kampeni zitafunguliwa Agosti Mosi hadi 6 na uchaguzi rasmi utafanyika Agosti 7.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship