January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Siasa yakunwa mradi wa TRA Sengerema

Na.Daud Magesa , Timesmajira Online, Sengerema

KAMATI ya Siasa Mkoa wa Mwanza imevutiwa na ujenzi wa ofisi za TRA Wilaya ya Sengerema kuwa umetekelezwa kwa weledi na viwango kulingana na thamani fedha.

Kauli hiyo imetolewa Mei 22,2024 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ baada ya Kamati ya Siasa kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni utekekezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020-2025.

Amesema mradi huo umetekelezwa kwa weledi,viwango na kwa wakati kulingana na thamani ya fedha hivyo utawezesha watumishi wa mamlaka hiyo kuhudumia wananchi na wafanyafabiashara katika mazingira bora.

‘Mradi huu umejengwa kwa viwango thamani ya fedha inaonekana kwa hatua ulipofikia unaridhisha bila kutia shaka kuwa fedha imetumika vibaya, Mkandarasi amefanya kazi nzuri ya kiwango na kwa wakati,”amesema Smart.

Mwenyekiti huyo wa CCM amesema kukamilika kwa jengo hilo wananchi watahudumiwa katika mazingira bora na serikali imeishasema wafanyabiashara wasifungiwe biashara, wenye changamoto wasilikilizwe na kodi wanazolipa zinaiwezesha serikali kutekekeza miradi ya maendeleo.

Meneja wa TRA Sengerema, Henry Raymond,amesema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya CF Builders kwa bilioni 3.5, mkandarasi ameshalipwa kiasi cha bilioni 1.36 sawa na asilimia 58 ya gharama za mradi wote.

Ameieleza Kamati hiyo ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mwanza kuwa, kazi za mradi huo zilizofanyika ni ujenzi wa miundombinu ya ofisi, umeme,maji, takwimu (Data -ICT), viyoyozi hivyo umefikia asilimia 85.

“Hatua ulipofikia, tunaahidi kuutekeleza haraka ili kukidhi mahitaji ya huduma ya kukusanya mapato ya serikali,”amesema Raymond.

Amesema vifaa vya miundombinu hiyo ya maji, umeme, data na viyoyozi havijafungwa huku mradi unakabiliwa na changamoto ya nyongeza ya kazi nje ya mkataba wa awali uwepo wa maji mengi chini ya ardhi (chemichemi kali), ufinyu wa eneo la kazi na mvua zinazoendelea kunyesha.

Katika hatua nyingine Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa imemtaka mkandarasi wa mradi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema,kuongeza kasi likamilike watumishi wafanye kazi katika mazingira mazuri na kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Tatizo ni muda wa utekelezaji wa mradi na malipo kuchelewa,ukiangalia fedha iliyowekwa na serikali katika mradi huu hauridhishi na mazingira hayafanani,hivyo usimamizi uongezwe kwa kuangalia thamani ya fedha,”amesema Smart na kushauri serikali itafute fedha mkandarasi alipwe mradi ukamilike.

Awali Mhandisi wa Halmashauri ya Sengerema, Elias Mwita katika taarifa kwa kamati hiyo ya siasa amesema mradi huo unaotekelezwa na SUMA JKT ulitakiwa kukamilika Juni 2024 lakini unasuasa.

Mradi huo unaogharimu zaidi ya bilioni 3 hadi sasa mkandarasi amelipwa bilioni 1.8,a unakabiliwa na changamoto ya mfumo ili kuwezesha malipo ya mkandarasi lakini pia mvua zimeathiri ujenzi wake.