Judith Ferdinand, Mwanza
Kamati ya kukusanya maoni juu ya usimamizi wa Hakimiliki Tanzania,imekutana na wadau wa Sanaa Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kukusanya maoni mbalimbali yatakayosaidia katika kutunga kanuni kufuatia mabadiliko ya sheria ya Hakimiliki na hakishiriki ya mwaka 1999.
Ambapo serikali kupitia mabadiliko ya sheria ya Fedha Julai,2022 imerekebisha sheria ya Hakimiliki na hakishiriki namba 7 ya mwaka 1999,ambapo wasanii kupitia kampuni zao wameruhusiwa kukusanya na kugawa mirahaba na cosota kubaki na jukumu la kusimamia hakimili nchini.
Akizungumza katika kikao cha kukusanya maoni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kukusanya maoni juu ya usimamizi wa kazi za Hakimiliki Dkt.Saudin Mwakaje, ameeleza kuwa wamekutana na wasanij wa sekta mbalimbali ili watoe maoni na mapendekezo ambayo watayapeleka serikalini na yatasaidia katika kutengeneza kanuni ambazo ni moja ya nyenzo muhimu ya utekelezaji wa mabadiliko ya sheria yaliofanyika mwaka huu.
Dkt Mwakaje ameeleza kupitia mabadiliko ya sheria hiyo ukusanyaji wa mirahaba utafanywa na kampuni binafsi ambazo zitakuwa zikisimamiwa na serikali katika utaratibu utakaowekwa na serikali katika kanuni ambazo zitatungwa hivi karibuni.
Pia imeweka tozo kwa vifaa vinavyotumika katika kubeba,kusambaza, kuhifadhi na kuzalisha kazi za ubunifu, pia imeweka adhabu ya kifungo cha miezi 6 mpaka miaka 3, ama faini isiyopungua milioni 20 au vyote Kwa pamoja kwa yule anayekiuka hakimili kwa mara ya kwanza.
“Vifaa vitalipiwa asilimia fulani ya kodi ambayo itaingizwa katika mfuko na itakuja kugawanywa kwa wasanii ikiwa ni wigo wa kuongeza makusanyo ya mirahaba ya kazi za wasanii na yanaboreshwa,”ameeleza Dkt Mwakaje.
Kwa upande wake Rais wa shirikisho la mziki Tanzania Addo November, ametia .apendekezo yake kwa kutaka mikataba iwe ya uwazi na ripoti ya ukusanyaji wa mirahaba itoke kila baada ya miezi mitatu na iwe ya uwazi.
Pia wanaokusanya mirabaha wawe na fedha ambazo wameweka kama ulinzi ambapo wakiharibu basi serikali isianze kuwatafuta na badala yake watumie zile fedha ambazo waliziweka.
Aidha November amependekeza fedha hizo zikusanywe kupitia vyombo vyote vya usafiri vya majini na nchi kavu kwa kulipia angalau kiasi kidogo kwa mwaka ambavyo vinatumia kazi za sanaa pia katika kumbi za starehe,sherehe.
“Cosota ijiridhishe na mikataba wanayoingia nayo wasanii kupitia lebo fulani ili kusaidia wasanii ambao wananyanyasika na iwe na ofisi nchi nzima kwa ngazi za mikoa yote na waongeze wanasheria na wafanyakazi, katika ugawaji wa mirabaha wapatiwe wasanii ambao wamesajiliwa na kiasi kikubwa cha fedha kiende kwa msanii husika huku kiasi kidogo kitumike kwa ajili ya kuendeshea ofisi,”ameeleza November.
Naye Mwenyekiti wa Producer Mkoa wa Mwanza,msanii wa filamu, Edward Kumalija, ameeleza kuwa ni vyema kwa ofisi za cosota ziwe kila mahali ili kuwezesha wasanii kupata huduma kutokana na changamoto iliopo ya ugumu wa kupata huduma kutoka kwa cosota kwa watu wa mikoani.
“Serikali itusaidie kwa kuhakikisha kazi ambazo hazijasajiliwa hazirushwi kwenye YouTube hiyo itasaidia kuwapata kazi ambazo hazijasajiliwa,”ameeleza Kumalija.
Aidha Richard Adams,amehoji kuwa suala la mirabaha ambayo ni mtu mmoja mmoja ananufaika itakuwaje Kwa wasanii wa filamu ambao wanashiriki watu wengi pamoja na kutatua changamoto ya vibali vingi Kwa wasanii wakati wakifanya shughuli zao.
Hata Hivyo Msanii wa maigizo mkoani Mwanza Peter Francis,ameiomba serikali kuwasaidia wasanii kupata na kujiendeleza kielimu Kwa gharama ndogo kwa kuanzisha chuo cha Sanaa Kanda ya Ziwa.
“Kanda ya Ziwa ni kubwa Ina mikoa 6 lakini haina chuo cha sanaa na nchi nzima kuna chuo kimoja cha sanaa,”ameeleza Francis.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato