November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya bunge yaridhishwa na kasi mradi kituo kupokea umeme Chalinze

Na Neema Mbuja, Chalinze

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara katika kituo cha kupokea na kupoza umeme Mkuwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze mkoani Pwani.

Meneja Mradi wa Kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze, Mha. Newton Livingstone akitoa maelezo ya mradi huo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walipotembelea mradi huo siku ya Ijumaa, 17 Machi 2023.

Pamoja na njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka katika mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kuja katika kituo hicho ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).Hivyo Kamati hiyo imeitaka Wizara ya Nishati pamoja na TANESCO kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati miradi hiyo miwili kabla ya kukamilika kwa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dustan Kitandula akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo,amesema kamati imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kuongeza kuwa itasaidia sana katika uwekezaji mkubwa na kukuza uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Maharage Chande akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walipotembelea kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze mkoani Pwani siku ya Ijumaa, 17 Machi 2023.

“Uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi sana sambamba na mahitaji ya upatikanaji wa nishati ya umeme hivyo TANESCO hakikisheni mnaweka msukumo mkubwa kwenye miradi hii,”amesema Kitandula.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema kukamilika kwa mradi huo wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze ambao unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia moja utanufaisha mikoa mbalimbali kwa kuongeza hali ya ubora na uhakika wa upatikanaji wa umeme wa uhakika utakaoingizwa katika Gridi ya Taifa.

Byabato ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuidhinisha fedha za kugharamia miradi hiyo ambapo hapo awali mradi huu wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze ulikuwa ufadhiliwe na mradi wa North Grid kabla ya serikali kuamua kuanza kuufadhili mradi huo kwa asilimia mia moja.

Naye Meneja mradi wa kituo hicho cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze, Mhandisi Newton Livingstone amesema kuwa mradi huo unajumuisha miradi miwili ambayo ni njia ya kusafirisha umeme mkubwa kutoka bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) hadi kituo cha Chalinze kwa msingi wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 160 wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 51.5.

Pamoja na kituo cha kupokea na kupoza umeme mkubwa wa kilovoti 400/220/132/33 cha Chalinze wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 44.06 kitakachohusisha ufungaji wa mashine mpya sita zenye uwezo wa Megavoti 250 kila moja.

Ujenzi huu wa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze kwa sasa umefikia asilimia 59 wakati kwa upande wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka JNHPP umefikia asilimia 92.