Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam.
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme inayotekelezwa kupitia TANESCO ambayo inakwenda kuondoa changamoto za umeme na kukuza uchumi wa nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dunstan Kitandula (Mbunge) wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia cha Kinyerezi 1,Machi 18,2023 mkoani Dar-es-,Salaam utakaozalisha jumla ya megawati 185.
“Kamati tumeona mradi unaendelea vizuri na mitambo mitatu tayari imeanza kuzalisha megawati 135 bado mtambo mmoja ambao utekelezaji wake unaendelea vizuri,”ameeleza Kitandula.
Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Jumla ya fedha zitakazotumika hadi mradi huu ukamilike ni dola za kimarekani milioni 188, hizi ni jitihada zake Rais,kwa ufadhili huu tuna uhakika utaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika wenye ubora na kuwezesha maendeleo mbalimbali kwenye viwanda vikubwa na vidogo na maendeleo ya kijamii,”ameeleza Byabato.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,Maharage Chande ameeleza kuwa mradi umepiga hatua kubwa tangu ulipoanza mwaka 2022 na mitambo mitatu kati ya minne ipo tayari na imeshaingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa.
Aidha, wajumbe wa Kamati hiyo Consatine Kanyasu (Mbunge) na Jesca David Kishoa (Mbunge viti maalum) wameipongeza Serikali ya awamu ya Sita kwa hatua zilizofikiwa kwenye mradi huo na wameiomba Serikali kutia mkazo kwenye kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato