Na WMJJWM-Dodoma
Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa, imeshauri agenda ya Kizazi chenye Usawa kujumiishwa katika Dira ya Taifa ya 2050 ili utekelezaji wake uwe katika mifumo ya utendaji wa Serikali.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Kamati hiyo kwa mkoa wa Dodoma Julai 09, 2024, yenye lengo la kufuatilia utekelezaji Programu ya Kizazi chenye Usawa na jitihada zilizopo katika Taasisi mbalimbali kukuza haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake nchini.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya ziara hiyo Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wake Mhe. Angellah Kairuki, Bi. Being’i Issa amesema suala la Usawa wa kijinsia ni mtambuka na linahitaji nguvu ya kila Taasisi kushirikiana na kuhakikisha linawekwa katika vipaumbele vyake ili kuwezesha kufikia ahadi zilizowekwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kufikia Kizazi chenye Usawa kiuchumi nchini.
“Niseme tu suala la Usawa wa kijinsia sio la Wizara moja au Taasisi moja ni letu sote na tukilibeba na kuliweka katika agenda za Kitaifa litaondoa ukakasi wa agenda hii kuonekana na ya upande wa jinsi moja tu bali ni kwa jinsi zote Wanawake kwa wanaume” amesisitiza Being’i.
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo Carolyn Kandusi ameshauri kuwepo na mikakati dhabiti katika Taasisi mbalimbali ili kuwe na mifumo itakayowezesha kuwepo na usawa wa kijinsia katika maeneo muhimu hasa katika sekta zenye kuwezesha wananchi kiuchumi.
Katibu wa Kikundi cha wajasiriamali cha Winni Star kilichonufaika wa uwezeshaji Wanawake kupitia asilimia kumi za Halmashauri, Julia Issaya Malabar amesema pamoja na kukumbana na changamoto mbalimbali hasa za kimtaji, wameungana na kujiwezesha kuanzisha biashara hiyo na baadae kuwezeshwa mkopo kutoka Halmashauri. Amewaasa Wanawake kuanza kujitoa ili juhudi zao ziweze kuungwa mkono na Serikali na wadau wengine wa maendeleo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika kiwanda cha uchakataji wa bidhaa za plastiki cha CAL Plastic Company Mmiliki wa Kiwanda hicho Aziza Abdi Hassir ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuwezesha kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mkopo kutoka Mfuko wa WDF uliofanikisha kukuza biashara yake hiyo.
“Nilianza na mtaji wa Millioni 9 kama fedha za uendeshaji na mpaka sasa nimefikia zaidi ya Millioni 100 na kuajiri watu kutoka sita mpaka zaidi ya 180 kwa kuzingatia Usawa wa kijinsia katika kutoa fursa za kiuchumi kupitia Kiwanda changu” alisisitiza Aziza
Kamati hiyo katika kufuatilia utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa siku ya kwanza kwa mkoa wa Dodoma imetembelea Kikundi cha wajasiriamali Wanawake cha Winning Star kilichopo Ilazo, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki kinachomilikiwa na Mwanamke Nala jijini Dodoma.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili