December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yatembelea kiwanda cha chai Mponde, waipongeza uwekezaji

NA MWANDISHI WETU, LUSHOTO

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, wametembelea kiwanda cha kuchakata Chai Mponde kilichoko Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga Machi 16, 2023 ili kukagua utekelezaji wa miradi mitano inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu (OWM-KVAU) na taasisi zilizo chini yake.

Kiwanda cha Chai Mponde kinamilikiwa kwa ubia na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) taassi ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu (OWK-KVAU),  kila taasisi inamiliki asilimia 42% ya hisa na Msajili wa Hazina(TR) asilimia 16%.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, Naibu wake Mhe. Patrobas Katambi, Katibu Mkuu Profesa Jamal Katundu na Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi hizo, CPA. Hosea Kashimba (PSSSF) na Dkt. John Mduma (WCF) pia walikuwepo wakati wa ziara hiyo.

Kiwanda cha Chai Mponde kilifanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kusimama kufanya kazi kwa kwa zaidi ya miaka 10, tayari kimeanza kazi ambapo kilo 24,460 zimeuzwa na tani 50 zinategemewa kuuzwa mwishoni mwa mwezi Machi, 2023.

Aidha Wajumbe wa Kamati wameipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuruhusu uwekezaji kwenye kiwanda hicho kwani kitanufaisha wakulima wa Chai wa Halmashauri ya Bumbuli na maeneo yanayozunguka wilaya nzima ya Lushoto.

“Kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kukubali uwekezaji huu, kwani unakwenda kuleta manufaa makubwa kwa wakulima wa chai.”Alisema Mhe. Fatma Tawfiq, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Aidha Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Riziki Lulida licha ya kupongeza alishauri uongozi wa kiwanda kutoa ajira kwa makundi mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu.

Akiongea kwa niaba ya wawekezaji Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema, kusudio kubwa la kukifufua kiwanda ni kuwawezesha wananchi wa Lushoto, Bumbuli Korogwe na maeneo jirani kupata kipato na hivyo kuwainua kiuchumi kwani wengi wanategemea zao hilo.

Meneja wa Kiwanda cha Chai Mponde, Bi.Sane Kwilabya (kulia) akiwapa maelezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu aina mbalimbali ya chai iliyochakatwa wakati wa ziara ya Kamati kwenye kiwanda hicho Machi 16, 2023.
Meneja wa Kiwanda cha Chai Mponde, Bi.Sane Kwilabya (kulia) akiwapa maelezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu kazi ya kuchakata chai inavyoendeswha wakati wa ziara ya Kamati kwenye kiwanda hicho Machi 16, 2023. Wakwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba.
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma akizunguzma mbele ya wajumbe.
Menyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Fatma Tawfiq (wapili kulia) na baadhi ya wajumbe w aKamati hiyo, wakiangalia chai ambayo tayari imechakatwa. Kushoto ni Meneja wa kiwanda cha Chai Mponde Bi. Sane Kwilabya.