Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, imetembelea Banda la Benki ya NMB katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nane Nane yanayofanyika jijini Mbeya, ambako pamoja na mambo mengine ilielezwa Mpango Mkakati wa taasisi hiyo katika kuwawezesha wadau wa Biashara, Kilimo na Mifugo kupitia mikopo ya riba nafuu.
Ikiongozwa na Mwenyekiti David Kihenzile ambaye ni Mbunge wa Mufindi Kusini mkoani Iringa na Makamu Mwenyekiti Mariam Ditopile, kamati hiyo ilielezwa ya kwamba licha ya kuwa NMB imeshatoa mikopo ya zaidi ya Sh. Trilioni 1.61 katika kipindi cha miaka sita, Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ni miongoni mwa Sekta za Kimkakati zinazopewa kipaumbele na NMB, kiasi cha kutengewa bajeti nono kila mwaka.
Meneja Uhusiano wa Kilimo Biashara wa NMB – Kanda ya Nyanda za Juu – Fabian Mnyanyika, ameieleza Kamati hiyo kuwa, licha ya benki yake kuwa ya kwanza kushusha riba ya mikopo ya Kilimo, Uvuvi, Ufugaji na misitu hadi kufikia asilimia 9 na kukopesha zaidi ya Sh. Trilioni 1.61 katika miaka sita, pia imetenga zaidi ya Sh. Bilioni 40 katika kipindi cha miaka miwili, Bil. 20 kati ya hizo ni kwa ajili ya kukopesha wadau wa Sekta hizo, huku Sh. Bilioni 20 zikiwa ni za mikopo ya ujenzi wa maghala Tanzania nzima.
Mnyanyika amebainisha kwamba, kumekuwa na mwitikio mkubwa miongoni mwa wakulima kukopa, ambako tayari wameshakopesha zaidi ya Sh. Bilioni 7 hadi Julai mwaka huu, ikiwemo mikopo inayohusisha pesa taslimu, pamoja na zana za Kilimo, Matrekta, ‘power tiller’ na pembejeo, kutoka Kampuni ya Agricom Africa, washirika wao wa kibiashara katika kuwakomboa wakulima nchini.
Akaongeza kuwa, katika msimu wa mavuno, wakulima wamevutiwa na kuchangamkia mikopo ya ujenzi wa maghala ili kukabiliana na upotevu na uharibifu wa mazao, ambako mkopaji anapaswa kuwa na kiwanja kilichopimwa, chenye hati Ili kukidhi matakwa ya kidhamana yaliyowekwa na benki hiyo, sambamba na kuahinisha thamani ya ghala analokusudia kujenga.
Mwenyekiti Kihenzile ameipongeza NMB sio tu kwa kuisapoti Serikali katika program ya kuandaa Vijana na Wanawake Kujenga Kesho Iliyo Bora (BBT), bali kwa kutenga mabilioni ya mikopo kwa wadau wa mnyororo huo wa thamani, pamoja na kushusha riba hadi asilimia 9 na kuzingatia nyakati sahihi za mkopaji kufanya marejesho.
More Stories
Wanafunzi 170 wapata ufadhili wa masomo
Maelfu kunufaika namsaada wa kisheria Katavi
Serikali yazidi kuwakosha wawekezaji wadau waipa tano