November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yaridhishwa maendeleo ya Nguru Hills

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Serikali kwa uwekezaji unaotia matumaini katika Machinjio ya kisasa ya Nguru Hills na kuishauri kuhakikisha nyama inayozaliswa katika kiwanda hicho inakubalika kimataifa ili kupata soko la uhakika haswa kwa soko la nje ya nchi.

Hayo yalisemwa na wajumbe mbalimbali wa kamati hiyo ya Bunge walipotembelea machinjio hayo ya kisasa yaliyopo Mvomero mkoani Morogoro.

Meneja Mkuu wa Machinjio ya kisasa ya Nguru yaliyoko Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro, Bw. Eric Cormack (kulia) akitoa maelezo kwa wajumbe Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii juu ya utendaji kazi katika machinjio hayo, wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya uwekezaji ya PSSSF Machi 14, 2023

Mradi wa Machinjio ya Nguru Hills unaendeshwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kushirikiana na Wabia wenza ambao ni Kampuni ya Eclipse Investiment LLC na Kampuni ya Busara Investment LLP

“Hongereni sana tumeona kazi hii nzuri, uwekezaji ni mzuri sana. Tunawapongeza, na pongezi za pekee kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake kubwa, tunamuombea nia yake nje kwa taifa letu ifanikiwe.Kwani uwekezaji huu ni matokeo ya sera nzuri za serilkali yetu.” Alisema Bibi. Fatma Tawfiq, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Mwenyekiti huyo aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kwa pamoja kuhakikisha wanaishauri serikali na wawekezaji wengine ili kiwanda hicho kithibitishwe kimataifa ili bidhaa zake ziweze kuuzwa katika soko lolote ulimwenguni.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo wakipatiwa maelezo ya ubora wa nyama ya Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills yanayomilikiwa na PSSSF huko Mvomero Mkoa wa Morogoro walipotembelea kukagua miradi ya uwekezaji inayotekelezwa na PSSSF kwa kushirikiana na wabia

Kwa upande wake, Mjumbe wa kamati hiyo ya Bunge, Mhe. Kabula Shitobelo alisema, “hongereni sana kiwanda ni kizuri sana tumekitembelea na tumeona jinsi kinavyofanya kazi”.

Mjumbe mwingine Mhe. Sophia Mwakagenda pamoja na kuridhishwa na uwekezaji huo ambao tayari umetoa ajira kwa vijana 300 alishauri kuwepo na usimamizi mzuri ili kiwanda kiwe na tija kwa taifa.

“Mradi huu unakwenda kuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji na wajasiriamali na wakiutumia vizuri utawasaidia kuongeza kipato” alisema Mjumbe mwingine Mhe. Neema Mwandabila.

Akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba, alisema katika kuhakikisha nyama ya Nguru inawafikia watanzania wengi kiwanda kina mpango wa kufungua maduka katika maeneo mbalimbali na kwa kuanzia duka limeshafunguliwa Morogoro mjini.

CPA. Kashimba alisema bidhaa zinazozalishwa katika machionjio ya kisasa ya Nguru zinaandaliwa kwa kufuata misingi ya imani za dini zote, hivyo walaji wasiwe na shaka na nyama inayotoka kiwandani hapo.

“Tunaishukuru kamati kwa kuamua kusaidia katika mchakato wa kupatikana kwa kibali cha bidhaa za kiwanda hiki kutambulimka kimataifa, kwa kweli tukipata ISO itakuwa rahisi sana kuuza bidhaa zetu popote pale Duniani.” Alisisitiza CPA Kashimba.

Akihitimisha ziara hiyo, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) aliishukuru kamati kwa kazi kubwa ya kukagua miradi iliyo chini ya Wizara hiyo na kwamba wamefarijika sana kwa ziara ya kamati hiyo.

“Tunahakikisha tunaendelea kusimamia kiwanda hiki ili fedha za wanachama zilizowekezwa hapa zifanye kazi iliyotarajiwa na hatimaye faida ipatikane ili wanachama waendelede kulipwa mafaoa yao” alisema Mhe. Ndalichako.