Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa – NHC kwa hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la Soko la Madini ya Tanzanite unaotekelezwa katika Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.
Akizungumza mara baada ya kutembelea jengo hilo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Timotheo Mzava – Mbunge wa Korogwe Vijijini amesema kuwa hali iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi huo ni nzuri na yakuridhisha na kwamba NHC inapaswa kupongezwa kwa juhudi inazofanya za kutekeleza mradi huo.
“Si mara yangu ya kwanza kutembelea miradi yenu kama hii ikiwemo ya ukandarasi na mara zote mmekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu vyema kwa kuwa mmeaminika nanyi mnajiaminisha kwa kujenga jengo zuri kubwa kama hili la Soko la Madini ya Tanzanite maana Kamati imeridhishwa na hatua iliyofikiwa na kwamba imani tuliyonayo ni mradi kukamilika kwa wakati katika kipindi kilichowekwa tena kwa ubora na thamani halisi ya mradi wenyewe” Alisema Mzava
Amebainisha kuwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina imani kubwa sana na NHC na ndio maana kila mara imekuwa haisiti kuwapatia miradi yake kwa ajili ya utekelezaji na hii inaashiria kuwa Shirika limejipanga vyema pamoja na mambo mengine kuhakikisha inatoa huduma bora kwa jamii.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Pinda (MB) amelipongeza shirika la Nyumba la Taifa kwa utekelezaji mahiri wa mradi wa Soko la Madini ya Tanzanite na kusema kuwa alama ambayo itaachwa na NHC katika mji wa Mirerani kwamwe haitofutika kwa wakazi wa eneo hili na wageni mbalimbali watakaofika katika soko hilo.
“NHC hongereni sana hamjaiangusha Wizara kwani Wajumbe wametoa shukrani nyingi za dhati basi tuendelee kufanya vyema katika miradi yetu yote ili tuwe namba moja katika miji yote ambako Shirika linatekeleza miradi yake. Pia sisi kama Wizara tutaendelea kuwasimamia na kuwaongoza vyema ili muendelee kuwa vinara katika sekta ya ujenzi” Alisema Naibu Waziri Pinda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NHC Dakta. Sophia Kongela aliishukuru Kamati hiyo kwa uamuzi wake wa kuja kutembelea mradi huo na kwamba maelekezo waliyoyatoa watayafanyia kazi ili kuendelea kuongeza ufanisi zaidi katika miradi ya Shirika.
Ujio wa Kamati hii ni fahari kubwa sana kwa Shirika kwani mawazo mnayoyatoa yanalisaidia Shirika katika kuhakikisha linatimiza wajibu wake ipasavyo na kwamba ziara hizi zimekuwa na tija sana kwa NHC. Hivyo niwakaribishe wakati mwingine mnapohitaji kutembelea miradi yetu mbalimbali kwani ushirikiano mnaotupatia unazidi kutuimarisha katika kutimiza majukumu yetu”
Wakichangia mara baada ya kusikiliza taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mhe. Neema Mgaya (Mbunge wa Viti Maalum Babati Mji) alisema kuwa NHC wamekuwa wazalendo kwani huwezi kwenda katika miradi wanayotekeleza ukakumbana na vitu visivyoeleweka daima wamekuwa wasafi katika miradi wanayotekeleza.
Mhe. Asia Halamga (Mbunge wa Viti Maalum -CCM) yeye alianza kwa kulishukuru Shirika kwa kujitoa kwa dhati katika kujenga jengo hilo ambalo kupitia michoro waliyoiona ni Dhahiri kuwa jengo hilo linakwenda kubadili taswira ya mji wa Mirerani kwani mpaka sasa hakuna jengo kubwa lililojengwa mahali hapo kama hilo la NHC.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah amesema kuwa awali NHC iliingia makubaliano ya kimkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ya ujenzi wa jengo la ghorofa tatu na kwamba wakati utekelezaji ukiendelea mshitiri aliiomba NHC wapitie mkataba wa awali ili kuliwezesha Shirika kujenga jengo lote mpaka ghorofa ya tano jambo ambalo lilizaa matunda na kwamba Shirika liko kwenye utekelezaji wa ujenzi wa jengo la ghorofa zote tano.
“Sisi Shirika tunaahidi kukamilisha ujenzi wa jengo hili kwa wakati tena kwa viwango na ubora unaotakiwa ili kuonesha thamani halisi ya fedha iliyotumika na kwamba huo ndiyo muelekeo wa NHC katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
Tunapata faraja kubwa sana mnapotupatia miongozo na maelekezo mbalimbali kwani inatusaidia katika kazi zetu na kuongeza ufanisi zaidi” Alisema Bw. Abdallah.
Akitoa majumuisho ya Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mwenyekiti wake Mhe. Mzava pamoja na mambo mengine kuwa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kwa kuichagua NHC kuwa mkandarasi na kusema kwamba Kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kuzitaka Taasisi zingine kuitumia NHC katika masuala ya ujenzi kwani wameonesha weledi mkubwa katika utekelezaji wa miradi waliyopewa na Serikali ikiwamo ya Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma na kwamba Kamati iko tayari kuisaidia NHC kupata eneo lolote linalohitaji kwa ajili ya uwekezaji nchini.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba