November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yampongeza Rais Samia kutekeleza miradi ya mageuzi kiuchumi

Na Mwandishi Wetu,Timemajiraonline

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti mwishoni mwa wiki imekagua
utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki
(EACOP) na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji miradi inayoleta mageuzi ya kiuchumi nchini.

Kamati hiyo ilitembelea kituo kitakachotumika kupokea, kuhifadhi na kusafirisha
mafuta ghafi kutoka Uganda ambapo wameahidi kuzidi kuupa msukumo mradi
huo wa kimkakati katika mageuzi ya kiuchumi.

Mara baada ya kukagua kituo hicho kilichopo Kata ya Chongoleani wilayani Tanga, Mkoa wa Tanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Oran Njeza amesema Kamati hiyo ambayo inasimamia mipango na uchumi wa nchi imeona mradi wa EACOP una umuhimu kiuchumi hivyo wataendelea kuupa msukumo mkubwa ili ukamilike kwa wakati.

Kamati hiyo ilimpongeza, Rais Dkt. Samia kwa mabadiliko ya kiuchumi anayoyafanya kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama wa EACOP ambayo inaendana na jinsi dunia inavyokwenda kwa sasa.

“Mradi mkubwa kama wa EACOP haukutegemewa kufanyika kwenye nchi za
Kiafrika, lakini maono ya viongozi wakuu wa nchi Uganda na Tanzania
yamepelekea mradi huu kufanyika ili kuwezesha mafuta sasa kusafirishwa
kwa njia ya mabomba ambayo pia yanasaidia katika ulinzi wa mazingira.”
aliesema Njeza

Aidha, Kamati hiyo ya Bajeti imeitaka Wizara ya Nishati kuweka
kipaumbele katika ujenzi wa mabomba yakayosafirisha nishati za aina
mbalimbali kama vile Gesi na Mafuta na hivyo kuifanya Tanzania kuwa
kituo cha usafirishaji wa nishati hizo barani Afrika.

Vilevile, Kamati imeliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) kuongeza nguvu ya kuutangaza mradi huo ili wananchi wafahamu
jinsi Serikali inavyoendelea kutekeleza miradi yake.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kuwa mradi
wa EACOP unafaida mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo kutoa ajira
takriban 900, kuongeza mzunguko wa fedha, kuongeza fursa za biashara
ikiwemo katika kituo cha kupokelea, kuhifadhi na kusafirikisha mafuta
kilichopo Chongoleani Tanga, kuuza rasilimali kama vile simenti na
kupata mapato mbalimbali kupitia ushuru.

Alitilia mkazo masuala ya afya na usalama pahala pa kazi katika miradi
mbalimbali nchini ambapo ameipongeza EACOP kwa kutekeleza suala hilo
kwa ufanisi ambapo katika masaa zaidi milioni mbili waliyofanya kazi
hakuna ajali iliyotokea kwenye maeneo yao ya kazi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio
alisema mradi wa EACOP ni wa kielelezo na kimkakati kutokana na
faida zake mbalimbali ikiwemo kuongeza mapato ya nchi katika kipindi
cha ujenzi na uendeshaji kwa kiasi cha sh.rilioni 2.3, kutoa
ajira kwa watanzania ambapo mpaka leo umeajiri takriban wananchi
7,584 huku ajira hizo zikitarajiwa kuongezeka.

Aliongeza kuwa, kampuni 146 za kitanzania zimehusika kutoa huduma
mbalimbali kwenye mradi na kunufaika kwa takriban Dola za Kimarekani
milioni 246 na pia mradi umepelekea kufanyika kwa manunuzi ya Dola za
Marekani milioni 462 pamoja na vijana wa kitanzania kupata mafunzo ya
teknolojia mbalimbali ambapo ujuzi huo watautumia kwenye miradi
mingine ya ujenzi wa mabomba kuelekea nchini Kenya na Zambia.

Alitaja wanahisa wa mradi huo kuwa ni Kampuni ya Total Energies ya
Ufaransa (62%), CNOOC ya China (8%), Kampuni ya Mafuta ya Uganda (15%)
na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (15%).

Alisema, kwa ujumla mradi unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia
39.2 huku baadhi ya kazi zikikamilika kwa asilimia 100 huku ujenzi wa
kiwanda cha kuwekea mabomba mfumo wa kuhifadhi joto cha Sojo ukifikia
asilimia 90 na katika eneo la Chongoleani mradi umefikia asilimia
takriban 40 na kueleza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni
mwaka 2026.

Alieleza kuwa, Serikali inashirikiana vizuri na wanahisa wengine
kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na Serikali ya Tanzania
imekamilisha kuchangia mtaji wake kama mwanahisa ambapo mpaka leo
Serikali.imechangia Dola za Marekani milioni 308 ambayo ni sawa na
asilimia 100 ya kiwango ambacho ni cha awali cha gharama za ujenzi kwa
asilimia 15 ya hisa za Tanzania.

Kuhusu utwaaji wa ardhi ya mkuza wa EACOP kwa upande wa Tanzania
alisema kuwa imekamilika kwa asilimia 99.2 na asilimia iliyobaki
inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo masuala ya mirathi. Amesema
kuwa kwa upande wa Uganda mradi huo pia unaendelea vizuri.