Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kigoma
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imeipongeza serikali kwa jitihada na utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme wa gridi ya taifa mkoani Kigoma, miradi inayotekelezwa kupitia Shirika la Umeme nchini TANESCO.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Jerry Slaa kwa niaba ya kamati, wakati wa ziara ya kukagua mashine za uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta katika kituo cha cha Bangwe mkoani Kigoma Machi 20, 2023 mashine zitakazozalisha jumla ya megawati 8.75.
Slaa, amesema kuwa serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha watanzania wanapata umeme wa uhakika kwa kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme na hasa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa njia ya umeme mkubwa wa kilovolt 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma,mradi ambao ukikamilika serikali itaweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika katika kuzalisha umeme kwa njia ya mafuta.
“uzalishaji wa umeme kwa mafuta ni dola senti 25 kwa unit,wa maji dola senti 5, umeme wa jua dola senti 4 na wa gesi ni dola senti 7 kwa unit moja tunaona kabisa uzalishaji wa mafuta unavyougharimu serikali” alisema Slaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande amesema kuwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovolti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma umekamilika kwa asilimia 47 na Kusema kuwa kazi ya kukamilisha mradi huo inaenda kwa kasi ili kuhakikisha mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani yanapata Umeme wa kutosha .
“mradi huu utakapokamilika tutazalisha umeme wa kutosha kuwasha Kigoma na kuweza kufanya biashara ya kuuza umeme nchi za jirani” aliongeza Chande
More Stories
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu
RC Mrindoko:Ufyekaji wa mahindi Tanganyika si maelekezo ya serikali