Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Bajeti, leo wamekagua utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika kituo kitakachotumika kupokea, kuhifadhi na kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda ambapo wameahidi kuzidi kuupa msukumo mradi huo wa kimkakati katika mageuzi ya kiuchumi.
Mara baada ya kukagua kituo hicho kilichopo Kata ya Chongoleani wilayani Tanga, Mkoa wa Tanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza amesema k itamati hiyo ambayo inasimamia mipango na uchumi wa nchi imeona mradi wa EACOP una umuhimu kiuchumi hivyo wataendelea kuupa msukumo mkubwa ili ukamilike kwa wakati.
Kamati hiyo imempongeza, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mabadiliko ya kiuchumi anayoyafanya kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama wa EACOP ambayo inaendana na jinsi dunia inavyokwenda kwa sasa.
“Mradi mkubwa kama wa EACOP haukutegemewa kufanyika kwenye nchi za kiafrika lakini maono ya Viongozi Wakuu wa nchi Uganda na Tanzania yamechangia mradi huu kufanyika ili kuwezesha mafuta kusafirishwa kwa njia ya mabomba ambayo pia yanasaidia katika ulinzi wa mazingira,”amesema Njeza.
Aidha, Kamati hiyo ya Bajeti imeitaka Wizara ya Nishati kuweka kipaumbele katika ujenzi wa mabomba yatakayosafirisha nishati za aina mbalimbali kama vile gesi na mafuta hivyo kuifanya Tanzania kuwa kituo cha usafirishaji wa nishati hizo barani Afrika.
Vilevile, Kamati imeliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuongeza nguvu ya kuutangaza mradi huo ili wananchi wafahamu jinsi Serikali inavyoendelea kutekeleza miradi yake.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian amesema kuwa mradi wa EACOP unafaida mbalimbali katika Mkoa huo ikiwemo kutoa ajira takribani 900.
Pia kuongeza mzunguko wa fedha na fursa za biashara ikiwemo kituo cha kupokelea, kuhifadhi na kusafirikisha mafuta kilichopo Chongoleani Tanga, kuuza rasilimali kama vile saruji na kupata mapato mbalimbali kupitia ushuru.
Ametilia mkazo masuala ya afya na usalama pahala pa kazi katika miradi mbalimbali nchini ambapo ameipongeza EACOP kwa kutekeleza suala hilo kwa ufanisi ambapo katika saa zaidi ya milioni mbili waliyofanya kazi hakuna ajali iliyotokea kwenye maeneo yao ya kazi.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema mradi wa EACOP ni wa kielelezo na kimkakati kutokana na faida zake mbalimbali ikiwemo kuongeza mapato ya nchi katika kipindi cha ujenzi na uendeshaji kwa kiasi cha trilioni 2.3, kutoa ajira kwa watanzania ambapo mpaka leo umeajiri takribani wananchi 7,584 huku ajira hizo zikitarajiwa kuongezeka.
Ameongeza kuwa, kampuni 146 za kitanzania zimehusika kutoa huduma mbalimbali kwenye mradi na kunufaika kwa takriban Dola za Kimarekani milioni 246.
Pia mradi umepelekea kufanyika kwa manunuzi ya Dola za Marekani milioni 462Â pamoja na vijana wa kitanzania kupata mafunzo ya teknolojia mbalimbali ambapo ujuzi huo watautumia kwenye miradi mingine ya ujenzi wa mabomba kuelekea maeneo mbalimbali kama Kenya na Zambia.
Ametaja wanahisa wa mradi huo kuwa ni kampuni ya Total Energies ya Ufaransa (62%), CNOOC ya China (8%), Kampuni ya Mafuta ya Uganda (15%) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (15%).
Amesema, kwa ujumla mradi unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 39.2 huku baadhi ya kazi zikikamilika kwa asilimia 100 ambapo ujenzi wa kiwanda cha kuwekea mabomba mfumo wa kuhifadhi joto cha sojo ukifikia asilimia 90 na katika eneo la Chongoleani mradi umefikia asilimia takribani 40 na kueleza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2026.
Ameeleza kuwa, Serikali inashirikiana vizuri na wanahisa wengine kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na Serikali ya Tanzania imekamilisha kuchangia mtaji wake kama mwanahisa.
Ambapo mpaka leo Serikali imechangia Dola za Marekani milioni 308 ambayo ni sawa na asilimia 100 ya kiwango ambacho ni cha awali cha gharama za ujenzi kwa asilimia 15 ya hisa za Tanzania.
Kuhusu utwaaji wa ardhi ya Mkuza wa EACOP kwa upande wa Tanzania amesema kuwa imekamilika kwa asilimia 99.2 na asilimia iliyobaki inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo masuala ya mirathi huku upande wa Uganda mradi huo pia unaendelea vizuri.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu