November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaliua yapitisha bajeti ya zaidi ya bilioni 45, mwaka wa fedha 2024/25

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora imepitisha mapendekezo ya bajeti ya maendeleo ya zaidi ya bil 45.8 zinazotarajiwa kukusanywa na kutumika kwa manufaa ya wananchi kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.

Hayo yamebainishwa Machi 4,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Jerry Daimon Mwaga alipokuwa akiwasilisha rasimu ya mpango wa maendeleo katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani.

Amebainisha kuwa wanatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha bil 7.04 kutoka vyanzo vya ndani huku Serikali Kuu ikitarajiwa kuwapatia kiasi cha sh bil 38.8 kwa ajili ya shughuli za maendeleo na matumizi mengine.

Mwaga amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri hiyo itatekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa huduma bora za kijamii na kiuchumi kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya 2025-2050.

Katika kutekeleza majukumu hayo halmashauri itazingatia mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka 5, malengo ya maendeleo endelevu na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 ili kuchochea kasi ya maendeleo kwa wananchi.

Pia amebainisha vipaumbele vya bajeti hiyo kuwa ni kuendelea kuboresha elimu ya msingi na sekondari kwa kuongeza miundombinu ya vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, vyoo, madawati na vitabu vya kutosha vya ziada na kiada.

Vipaumbele vingine ni kuongeza idadi ya shule za msingi na sekondari ili kupunguza umbali kwa watoto, kukamilisha miundombinu iliyoanza kujengwa katika shule mbalimbali na kuhakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari.

Mwaga amesisitiza kuwa wataendelea kutekeleza adhima ya serikali ya kuhakikisha kila Tarafa inakuwa na shule ya kidato cha 5 na 6 ili kupanua wigo wa elimu na kuwezesha watoto wote kupata fursa ya elimu.

Ameongeza kuwa mikakati mingine ni kuboresha huduma za afya kwa kuongeza zahanati na vituo vya afya pamoja na kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana, kudhibiti magonjwa ya mlipuko na maambukizi ya VVU.

Pia wataendelea kuboresha sekta ya kilimo na mifugo kwa kuimarisha huduma za usimamizi ili kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao mbalimbali ya chakula na biashara ili kuinua maisha ya wakulima na wafugaji.

Mikakati mingine ni kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato, kuimarisha mfumo wa sheria na utawala bora, kuimarisha shughuli za utamaduni na michezo, kuimarisha utunzaji mazingira na kuratibu uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Japhael Lufungija amebainisha kuwa wao ni mfano wa kuigwa na halmashauri zingine za Mkoa huo kutokana na kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato ambayo hupelekea kuvuka lengo kila mwaka.

Ametoa wito kwa Watendaji na Maofisa wote waliopewa dhamana ya kukusanya mapato kuhakikisha kasi hii inaendelezwa na kuelekeza mapato yote yapelekwe benki kwa wakati kinyume na hapo watashughulikiwa.

Aidha amempongeza Mkurugenzi kwa dhamira yake ya kupandisha vyeo watumishi 1,744, kubadilishia miundo ya utumishi watumishi 3 na kuajiri watumishi wapya 395 kwa mwaka huu wa fedha 2024/25 ili kuleta mabadiliko chanya katika ustawi wa jamii.