January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaliua wajipanga kutokomeza maambukizi ya VVU

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI ya Wilaya Kaliua Mkoani Tabora imedhamiria kutokomeza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa wakazi wake kwa kuhakikisha huduma stahiki inatolewa kwa wenye maambukizi wote, kupanua wigo wa upimaji na kuongeza vituo vya kutolea huduma hiyo katika vijiji na kata zote.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Japhael Lufungija alipokuwa akiongea na madiwani, watumishi na watendaji wa kata katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo jana.

Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea zaidi ya sh mil 200 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya na upatikanaji huduma zote hivyo akabainisha kuwa hakuna sababu ya watu wenye VVU kukosa huduma tena.

Amebainisha kuwa takwimu za kiutafiti za Ukimwi zinaonesha kuwa kwa mwaka 2016/2017 maambukizi Kimkoa ilikuwa asilimia 5.1 na mwaka 2022/2023 ilikuwa asilimia 5.6, hivyo akasisitiza dhamira ya halmashauri kudhibiti maambukizi yote.

‘Tumejipanga kutokomeza ugonjwa wa Ukimwi katika Wilaya yetu, wito wangu kwa wananchi kila mmoja ajenge utamadauni wa kupima afya yake ili atakapobainika kuwa na maambukizi aanze kupatiwa huduma mara moja’, amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Ukimwi Fabian Buluba (diwani wa kata ya Sasu) ametaja baadhi ya Mikakati ya halmashauri hiyo kuwa ni kutoa elimu ya kujilinda na kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kugawa kondomu bure katika nyumba zote za kulala wageni.

Mkakati mwingine ni kuongeza vituo vya kutolea huduma za kliniki (CTC) kwa wale wote waliogundulika kuwa na maambukizi ya VVU na kuhakikisha asilimia 95 wanatumia dawa pia wataweka utaratibu wa kuwapima ili kutambua hali zao.

Aidha amebainisha kuwa watahakikishia asilimia 95 ya wale wote watakaoanza kutumia dawa wanazitumia vizuri kwa asilimia 95 na virusi vilivyoko mwilini vinashuka chini ya kopi 1000 kwa kupimwa.